Sefania 2
1 Jikusanyeni, naam, jikusanyeni, Ee taifa lisilo na haya;
2 kabla haijazaa hiyo amri, kabla haijapita siku ile kama makapi, kabla haijawajilia hasira kali ya Bwana, kabla haijawajilia siku ya hasira ya Bwana.
3 Mtafuteni Bwana, enyi nyote mlio wanyenyekevu wa dunia, ninyi mliozitenda hukumu zake; itafuteni haki, utafuteni unyenyekevu; huenda mtafichwa katika siku ya hasira ya Bwana.
4 Kwa kuwa Gaza utaachwa, na Ashkeloni utakuwa ukiwa; wataufukuzia mbali Ashdodi wakati wa adhuhuri, na Ekroni utang'olewa.
5 Ole wao wakaao karibu na pwani ya bahari, taifa la Wakerethi! Neno la Bwana li juu yenu, Ee Kanaani, nchi ya Wafilisti; mimi nitakuangamiza, asibaki mtu akaaye kwako.
6 Na hiyo nchi ya pwani itakuwa malisho, yenye vibanda vya wachungaji, na mazizi ya makundi ya kondoo.
7 Na hiyo nchi ya pwani itakuwa nchi ya watu wa nyumba ya Yuda waliosalia; watalisha makundi yao huko; watalala katika nyumba za Ashkeloni wakati wa jioni; kwa maana Bwana, Mungu wao, atawajilia na kuwarudisha wafungwa wao.
8 Mimi nimeyasikia matukano ya Moabu, na dhihaka za wana wa Amoni, ambazo kwa hizo wamewatukana watu wangu, na kujitukuza juu ya mpaka wao.
9 Basi kama niishivyo, asema Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, Hakika Moabu atakuwa kama Sodoma, na wana wa Amoni kama Gomora, yaani, milki ya upupu, na mashimo ya chumvi, ukiwa wa daima; watu wangu waliosalia watawateka nyara, na watu wa taifa langu waliobaki watawarithi.
10 Mambo hayo yatawapata kwa sababu ya kiburi chao, kwa kuwa wamewatukana watu wa Bwana wa majeshi, na kujitukuza juu yao.
11 Bwana atakuwa mwenye kuwatisha sana; kwa maana atawafisha kwa njaa miungu yote ya dunia; na watu watamsujudia yeye, kila mtu toka mahali pake; naam, nchi zote za mataifa.
12 Na ninyi Wakushi pia, mtauawa kwa upanga wangu.
13 Naye atanyosha mkono wake juu ya upande wa kaskazini, na kuiangamiza Ashuru; naye ataufanya Ninawi kuwa ukiwa, kuwa mahali pakavu kama jangwa.
14 Na makundi ya wanyama watalala kati yake, wanyama wote wa mataifa; mwari-nyuni na nungu watakaa juu ya vichwa vya nguzo zake; sauti yao itasikiwa madirishani; vizingitini mwake mtakuwa ukiwa; kwa maana ameifunua kazi ya mierezi.
15 Huu ndio mji ule wa furaha, Uliokaa pasipo kufikiri, Uliosema moyoni mwake, Mimi niko, Wala hapana mwingine ila mimi. Jinsi ulivyokuwa ukiwa, Mahali pa kulala pa wanyama wa bara! Kila mtu apitaye atazomea, Na kutikisa mkono wake.