Zekaria 7
1 Ikawa katika mwaka wa nne wa mfalme Dario, neno la Bwana lilimjia Zekaria, siku ya nne ya mwezi wa kenda, yaani, Kisleu.
2 Basi watu wa Betheli walikuwa wamewatuma Shareza na Regem-meleki, na watu wao, ili kuomba fadhili za Bwana,
3 na kusema na makuhani wa nyumba ya Bwana wa majeshi, na hao manabii, ya kwamba, Je! Yanipasa kulia katika mwezi wa tano, na kujitenga na watu, kama nilivyofanya miaka hii mingi iliyopita?
4 Ndipo neno la Bwana wa majeshi likanijia, kusema,
5 Waambie watu wote wa nchi, na hao makuhani, ukisema, Hapo mlipofunga na kuomboleza katika mwezi wa tano na mwezi wa saba, katika miaka hiyo sabini, je! Mlinifungia mimi kwa lo lote; mlinifungia mimi?
6 Na wakati mlapo chakula na kunywa, je! Hamli kwa ajili ya nafsi zenu, na kunywa kwa ajili ya nafsi zenu?
7 Je! Hayo siyo maneno aliyoyasema Bwana kwa vinywa vya manabii wa zamani, wakati Yerusalemu ulipokaliwa na watu na kufanikiwa, na miji yake iliyokuwa ikiuzunguka; na wakati ule ambao nchi ya Negebu na Shefela ilipokuwa ikikaliwa na watu?
8 Kisha neno la Bwana likamjia Zekaria, kusema,
9 Bwana wa majeshi amesema hivi, ya kwamba, Fanyeni hukumu za kweli, kila mtu na amwonee ndugu yake rehema na huruma;
10 tena msimdhulumu mjane, wala yatima, wala mgeni, wala maskini; wala mtu awaye yote miongoni mwenu asiwaze mabaya juu ya ndugu yake moyoni mwake.
11 Lakini hao walikataa kusikiliza, wakageuza bega lao, wakaziba masikio yao ili wasisikie.
12 Naam, walifanya mioyo yao kuwa kama jiwe gumu, wasije wakaisikia sheria na maneno ya Bwana wa majeshi, aliyoyapeleka kwa roho yake kwa mkono wa manabii wa kwanza; kwa sababu hiyo ghadhabu kuu ikatoka kwa Bwana wa majeshi.
13 Ikawa kwa sababu alilia, wao wasitake kusikiliza; basi, wao nao watalia, wala mimi sitasikiliza, asema Bwana wa majeshi.
14 Lakini nitawatawanya kwa upepo wa kisulisuli, katikati ya mataifa yote wasiowajua. Basi hivyo ndivyo ilivyokuwa ukiwa nchi baada yao, hata hapakuwa na mtu aliyepita kati yake, wala aliyerudi; maana waliifanya nchi iliyopendeza sana kuwa ukiwa.