Zekaria 5
1 Basi, nikainua macho yangu tena, nikaona, na tazama, gombo la chuo lirukalo.
2 Akaniuliza, Unaona nini? Nikajibu, Naona gombo la chuo lirukalo; na urefu wake ni dhiraa ishirini, na upana wake dhiraa kumi.
3 Ndipo akaniambia, Hii ndiyo laana itokayo kwenda juu ya uso wa nchi yote; maana kwa hiyo kila aibaye atatolewa kama ilivyo upande mmoja, na kwa hiyo kila aapaye atatolewa kama ilivyo upande wa pili.
4 Nitaituma itokee, asema Bwana wa majeshi, nayo itaingia katika nyumba ya mwivi, na katika nyumba yake yeye aapaye kwa uongo kwa jina langu; nayo itakaa katikati ya nyumba yake, na kuiteketeza, pamoja na boriti zake na mawe yake.
5 Ndipo yule malaika aliyesema nami akatokea, akaniambia, Inua macho yako sasa, uone ni kitu gani kitokeacho.
6 Nikasema, Ni kitu gani? Akasema, Kitu hiki ni efa itokeayo. Tena akasema, Huu ndio uovu wao katika nchi hii yote;
7 na tazama, talanta ya risasi iliinuliwa; na tazama, mwanamke akaaye katikati ya hiyo efa.
8 Akasema, Huyu ni Uovu; akamtupa chini katikati ya ile efa; akalitupa lile jiwe la risasi juu ya mdomo wa ile efa.
9 Ndipo nikainua macho yangu, nikaona, na tazama, wanawake wawili walitokea, nao upepo ulikuwa katika mabawa yao; na mabawa yao yalikuwa kama mabawa ya korongo; wakaiinua ile efa kati ya dunia na mbingu.
10 Ndipo nikamwambia yule malaika aliyesema nami, Hawa wanaipeleka wapi efa hii?
11 Akaniambia, Wanakwenda kumjengea nyumba katika nchi ya Shinari; tena ikiisha kutengenezwa, atawekwa huko mahali pake mwenyewe.