Ufunuo 17
1 Akaja mmoja wa wale malaika saba, wenye vile vitasa saba, akanena nami, akisema, Njoo huku, nitakuonyesha hukumu ya yule kahaba mkuu aketiye juu ya maji mengi;
2 ambaye wafalme wa nchi wamezini naye, nao wakaao katika nchi wamelevywa kwa mvinyo ya uasherati wake.
3 Akanichukua katika Roho hata jangwani, nikaona mwanamke, ameketi juu ya mnyama mwekundu sana, mwenye kujaa majina ya makufuru, mwenye vichwa saba na pembe kumi.
4 Na mwanamke yule alikuwa amevikwa nguo ya rangi ya zambarau, na nyekundu, amepambwa kwa dhahabu, na kito cha thamani, na lulu, naye alikuwa na kikombe cha dhahabu mkononi mwake, kilichojawa na machukizo, na machafu ya uasherati wake.
5 Na katika kipaji cha uso wake alikuwa na jina limeandikwa, la siri, BABELI MKUU, MAMA WA MAKAHABA NA MACHUKIZO YA NCHI.
6 Nikamwona yule mwanamke amelewa kwa damu ya watakatifu, na kwa damu ya mashahidi wa Yesu. Nami nilipomwona nikastaajabu ajabu kuu.
7 Na yule malaika akaniambia, Kwani kustaajabu? Nitakuambia siri ya mwanamke huyu, na ya mnyama huyu amchukuaye, mwenye vile vichwa saba na zile pembe kumi.
8 Yule mnyama uliyemwona alikuwako, naye hayuko, naye yu tayari kupanda kutoka kuzimu na kwenda kwenye uharibifu. Na hao wakaao juu ya nchi, wasioandikwa majina yao katika kitabu cha uzima tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu, watastaajabu wamwonapo yule mnyama, ya kwamba alikuwako, naye hayuko, naye atakuwako.
9 Hapo ndipo penye akili zenye hekima. Vile vichwa saba ni milima saba anayokalia mwanamke huyo.
10 Navyo ni wafalme saba. Watano wamekwisha kuanguka, na mmoja yupo, na mwingine hajaja bado. Naye atakapokuja imempasa kukaa muda mchache.
11 Na yule mnyama aliyekuwako naye hayuko, yeye ndiye wa nane, naye ni mmoja wa wale saba, naye aenenda kwenye uharibifu.
12 Na zile pembe kumi ulizoziona ni wafalme kumi, ambao hawajapokea ufalme bado, lakini wapokea mamlaka kama wafalme muda wa saa moja pamoja na yule mnyama.
13 Hawa wana shauri moja, nao wampa yule mnyama nguvu zao na mamlaka yao.
14 Hawa watafanya vita na Mwana-Kondoo, na Mwana Kondoo atawashinda, kwa maana Yeye ni Bwana wa Mabwana, na Mfalme wa Wafalme, na hao walio pamoja naye ndio walioitwa, na wateule, na waaminifu.
15 Kisha akaniambia, Yale maji uliyoyaona, hapo aketipo yule kahaba, ni jamaa na makutano na mataifa na lugha.
16 Na zile pembe kumi ulizoziona, na huyo mnyama, hao watamchukia yule kahaba, nao watamfanya kuwa mkiwa na uchi, watamla nyama yake, watamteketeza kabisa kwa moto.
17 Maana Mungu ametia mioyoni mwao kufanya shauri lake, na kufanya shauri moja, na kumpa yule mnyama ufalme wao hata maneno ya Mungu yatimizwe.
18 Na yule mwanamke uliyemwona, ni mji ule mkubwa, wenye ufalme juu ya wafalme wa nchi.