Ufunuo 16
1 Nikasikia sauti kuu kutoka hekaluni, ikiwaambia wale malaika saba, Enendeni, mkavimimine vile vitasa saba vya ghadhabu ya Mungu juu ya nchi.
2 Akaenda huyo wa kwanza, akakimimina kitasa chake juu ya nchi; pakawa na jipu baya, bovu, juu ya wale watu wenye chapa ya huyo mnyama, na wale wenye kuisujudia sanamu yake.
3 Na huyo wa pili akakimimina kitasa chake juu ya bahari, ikawa damu kama damu ya mfu, na vitu vyote vyenye roho ya uhai katika bahari vikafa.
4 Na huyo wa tatu akakimimina kitasa chake juu ya mito na chemchemi za maji; zikawa damu.
5 Nami nikamsikia malaika wa maji akisema, Wewe u mwenye haki, uliyeko na uliyekuwako, Mtakatifu, kwa kuwa umehukumu hivi;
6 kwa kuwa walimwaga damu ya watakatifu na ya manabii, nawe umewapa damu wainywe; nao wamestahili.
7 Nikaisikia hiyo madhabahu ikisema, Naam, Bwana Mungu Mwenyezi, ni za kweli, na za haki, hukumu zako.
8 Na huyo wa nne akakimimina kitasa chake juu ya jua, nalo likapewa kuwaunguza wanadamu kwa moto.
9 Wanadamu wakaunguzwa maunguzo makubwa, nao wakalitukana jina la Mungu aliye na mamlaka juu ya mapigo hayo; wala hawakutubu wala kumpa utukufu.
10 Na huyo wa tano akakimimina kitasa chake juu ya kiti cha enzi cha yule mnyama; ufalme wake ukatiwa giza; wakatafuna ndimi zao kwa sababu ya maumivu,
11 wakamtukana Mungu wa mbingu kwa sababu ya maumivu yao, na kwa sababu ya majipu yao; wala hawakuyatubia matendo yao.
12 Na huyo wa sita akakimimina kitasa chake juu ya mto ule mkubwa Frati; maji yake yakakauka, ili njia itengenezwe kwa wafalme watokao katika maawio ya jua.
13 Nikaona roho tatu za uchafu zilizofanana na vyura, zikitoka katika kinywa cha yule joka, na katika kinywa cha yule mnyama, na katika kinywa cha yule nabii wa uongo.
14 Hizo ndizo roho za mashetani, zifanyazo ishara, zitokazo na kuwaendea wafalme wa ulimwengu wote kuwakusanya kwa vita ya siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi.
15 (Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake.)
16 Wakawakusanya hata mahali paitwapo kwa Kiebrania, Har-Magedoni.
17 Na huyo wa saba akakimimina kitasa chake juu ya anga. Sauti kuu ikatoka katika hekalu, katika kile kiti cha enzi, ikisema, Imekwisha kuwa.
18 Pakawa na umeme na sauti na radi; na palikuwa na tetemeko la nchi kubwa, ambalo tangu wanadamu kuwako juu ya nchi hapakuwa namna ile, jinsi lilivyokuwa kubwa tetemeko hilo.
19 Na mji ule mkuu ukagawanyikana mafungu matatu, na miji ya mataifa ikaanguka; na Babeli ule mkuu ukakumbukwa mbele za Mungu, kupewa kikombe cha mvinyo ya ghadhabu ya hasira yake.
20 Kila kisiwa kikakimbia, wala milima haikuonekana tena.
21 Na mvua ya mawe kubwa sana, ya mawe mazito kama talanta, ikashuka kutoka mbinguni juu ya wanadamu. Wanadamu wakamtukana Mungu kwa sababu ya lile pigo la mvua ya mawe; kwa maana pigo lake ni kubwa mno.