Zaburi 98
1 Mwimbieni Bwana wimbo mpya, Kwa maana ametenda mambo ya ajabu. Mkono wa kuume wake mwenyewe, Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu.
2 Bwana ameufunua wokovu wake, Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
3 Amezikumbuka rehema zake, Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli. Miisho yote ya dunia imeuona Wokovu wa Mungu wetu.
4 Mshangilieni Bwana, nchi yote, Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi.
5 Mwimbieni Bwana zaburi kwa kinubi, Kwa kinubi na sauti ya zaburi.
6 Kwa panda na sauti ya baragumu. Shangilieni mbele za Mfalme, Bwana.
7 Bahari na ivume na vyote viijazavyo, Ulimwengu nao wanaokaa ndani yake.
8 Mito na ipige makofi, Milima na iimbe pamoja kwa furaha.
9 Mbele za Bwana; Kwa maana anakuja aihukumu nchi. Atauhukumu ulimwengu kwa haki, Na mataifa kwa adili.