«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »

Zaburi 86

1  Ee Bwana, utege sikio lako unijibu, Maana mimi ni maskini na mhitaji

2  Unihifadhi nafsi yangu, Maana mimi ni mcha Mungu. Wewe uliye Mungu wangu, Umwokoe mtumishi wako anayekutumaini.

3  Wewe, Bwana, unifadhili, Maana nakulilia Wewe mchana kutwa.

4  Uifurahishe nafsi ya mtumishi wako, Maana nafsi yangu nakuinulia Wewe, Bwana.

5  Kwa maana Wewe, Bwana, U mwema, Umekuwa tayari kusamehe, Na mwingi wa fadhili, Kwa watu wote wakuitao.

6  Ee Bwana, uyasikie maombi yangu; Uisikilize sauti ya dua zangu.

7  Siku ya mateso yangu nitakuita, Kwa maana utaniitikia.

8  Katikati ya miungu hakuna kama Wewe, Bwana, Wala matendo mfano wa matendo yako.

9  Mataifa yote uliowafanya watakuja; Watakusujudia Wewe, Bwana, Watalitukuza jina lako;

10  Kwa kuwa ndiwe uliye mkuu, Wewe ndiwe mfanya miujiza, Ndiwe Mungu peke yako.

11  Ee Bwana, unifundishe njia yako; Nitakwenda katika kweli yako; Moyo wangu na ufurahi kulicha jina lako;

12  Nitakusifu Wewe, Bwana, Mungu wangu, Kwa moyo wangu wote, Nitalitukuza jina lako milele.

13  Maana fadhili zako kwangu ni nyingi sana; Umeiopoa nafsi yangu na kuzimu.

14  Ee Mungu, wenye kiburi wamenishambulia; Mkutano wa wakatili wamenitafuta roho. Wala hawakukuweka Wewe Mbele ya macho yao.

15  Lakini Wewe, Bwana, U Mungu wa rehema na neema, Mvumilivu, mwingi wa fadhili na kweli.

16  Unielekee na kunifadhili mimi; Mpe mtumishi wako nguvu zako, Umwokoe mwana wa mjakazi wako.

17  Unifanyie ishara ya wema, Wanichukiao waione na kuaibishwa. Kwa kuwa Wewe, Bwana, Umenisaidia na kunifariji.

«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »
“Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi.” — 1 Wakorintho 16:23