Zaburi 66
1 Mpigie Mungu kelele za shangwe, nchi yote,
2 Imbeni utukufu wa jina lake, Tukuzeni sifa zake.
3 Mwambieni Mungu, Matendo yako yatisha kama nini! Kwa ajili ya wingi wa nguvu zako, Adui zako watakuja kunyenyekea mbele zako.
4 Nchi yote itakusujudia na kukuimbia, Naam, italiimbia jina lako.
5 Njoni yatazameni matendo ya Mungu; Hutisha kwa mambo awatendayo wanadamu;
6 Aligeuza bahari ikawa nchi kavu; Katika mto walivuka kwa miguu; Huko ndiko mlikomfurahia.
7 Atawala kwa uweza wake milele; Macho yake yanaangalia mataifa; Waasio wasijitukuze nafsi zao.
8 Enyi mataifa, mtukuzeni Mungu wetu, Itangazeni sauti ya sifa zake;
9 Aliyeiweka nafsi yetu katika uhai, Wala hakuuacha mguu wetu usogezwe.
10 Kwa maana umetupima, Ee Mungu, Umetujaribu inavyojaribiwa fedha.
11 Ulituingiza ndani ya wavu, Na kuweka viunoni mwetu mzigo uliotulemea.
12 Uliwapandisha watu Juu ya vichwa vyetu. Tulipita motoni na majini; Ukatutoa na kutuleta kunako wingi.
13 Nitaingia nyumbani mwako na kafara; Nitaondoa kwako nadhiri zangu;
14 Ambazo midomo yangu ilizinena; Kinywa changu kikazisema nilipokuwa taabuni.
15 Kafara za vinono nitakutolea, Pamoja na fukizo la kondoo waume, Nitatoa ng'ombe pamoja na mbuzi.
16 Njoni, sikieni, ninyi nyote mnaomcha Mungu, Nami nitayatangaza aliyonitendea roho yangu.
17 Nalimwita kwa kinywa changu, Na sifa kuu zilikuwa chini ya ulimi wangu.
18 Kama ningaliwaza maovu moyoni mwangu, Bwana asingesikia.
19 Hakika Mungu amesikia; Ameisikiliza sauti ya maombi yangu.
20 Na ahimidiwe Mungu asiyeyakataa maombi yangu, Wala kuniondolea fadhili zake.