«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »

Zaburi 65

1  Ee Mungu, sifa zakulaiki katika Sayuni, Na kwako Wewe itaondolewa nadhiri.

2  Wewe usikiaye kuomba, Wote wenye mwili watakujia.

3  Ingawa maovu mengi yanamshinda, Wewe utayafunika maasi yetu.

4  Heri mtu yule umchaguaye, Na kumkaribisha akae nyuani mwako. Na tushibe wema wa nyumba yako, Patakatifu pa hekalu lako.

5  Kwa mambo ya kutisha utatujibu, Katika haki, Ee Mungu wa wokovu wetu. Wewe uliye tumaini la miisho yote ya dunia, Na la bahari iliyo mbali sana,

6  Milima waiweka imara kwa nguvu zako, Huku ukijifunga uweza kama mshipi.

7  Wautuliza uvumi wa bahari, Uvumi wa mawimbi yake, Na ghasia ya mataifa;

8  Kwa hiyo wakaao mbali kabisa huogopa ishara zako; Milango ya asubuhi na jioni waifurahisha.

9  Umeijilia nchi na kuisitawisha, Umeitajirisha sana; Mto wa Mungu umejaa maji; Wawaruzuku watu nafaka Maana ndiwe uitengenezaye ardhi.

10  Matuta yake wayajaza maji; Wapasawazisha palipoinuka, Wailainisha nchi kwa manyunyu; Waibariki mimea yake.

11  Umeuvika mwaka taji ya wema wako; Mapito yako yadondoza unono.

12  Huyadondokea malisho ya nyikani, Na vilima vyajifunga furaha.

13  Na malisho yamevikwa kondoo, Na mabonde yamepambwa nafaka, Yanashangilia, naam, yanaimba.

«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »
“Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi.” — 1 Wakorintho 16:23