Zaburi 64
1 Mungu, uisikie sauti yangu katika malalamiko yangu; Unilinde uhai wangu na hofu ya adui.
2 Utanificha mbali na shauri la siri la watenda mabaya, Mbali na ghasia ya watu wafanyao maovu;
3 Waliounoa ulimi wao kama upanga, Wameielekeza mishale yao, maneno ya uchungu,
4 Wapate kumpiga mkamilifu faraghani, Kwa ghafula humpiga wala hawaogopi.
5 Walijifanya hodari katika jambo baya; Hushauriana juu ya kutega mitego; Husema, Ni nani atakayeiona?
6 Hutunga maovu; husema, Tumefanya shauri kamili; Na mawazo ya ndani ya kila mmoja wao, Na moyo wake, huwa siri kabisa.
7 Kwa hiyo Mungu atawapiga shabaha, Kwa mshale mara watapigwa.
8 Ndivyo watakavyokwazwa, Ulimi wao wenyewe ukishindana nao. Wote wawaonao watatikisa kichwa.
9 Na watu wote wataogopa, Wataitangaza kazi ya Mungu, Na kuyafahamu matendo yake.
10 Mwenye haki atamfurahia Bwana na kumkimbilia, Na wote wenye moyo wa adili watajisifu.