«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »

Zaburi 63

1  Ee MUNGU, Mungu wangu, nitakutafuta mapema, Nafsi yangu inakuonea kiu, Mwili wangu wakuonea shauku, Katika nchi kame na uchovu, isiyo na maji.

2  Ndivyo nilivyokutazama katika patakatifu, Nizione nguvu zako na utukufu wako.

3  Maana fadhili zako ni njema kuliko uhai; Midomo yangu itakusifu.

4  Ndivyo nitakavyokubariki maadamu ni hai; Kwa jina lako nitaiinua mikono yangu.

5  Nafsi yangu itakinai kama kushiba mafuta na vinono; Kinywa changu kitakusifu kwa midomo ya furaha.

6  Ninapokukumbuka kitandani mwangu, Nakutafakari Wewe makesha yote ya usiku.

7  Maana Wewe umekuwa msaada wangu, Na uvulini mwa mbawa zako nitashangilia.

8  Nafsi yangu inakuandama sana; Mkono wako wa kuume unanitegemeza.

9  Bali waitafutao nafsi yangu, ili kuiharibu, Wataingia pande za nchi zilizo chini.

10  Watatolewa wafe kwa nguvu za upanga, Watakuwa riziki za mbwa-mwitu.

11  Bali mfalme atamfurahia Mungu, Kila aapaye kwa Yeye atashangilia, Kwa maana vinywa vya waongo vitafumbwa.

«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »
“Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi.” — 1 Wakorintho 16:23