Zaburi 62
1 Nafsi yangu yamngoja Mungu peke yake kwa kimya, Wokovu wangu hutoka kwake.
2 Yeye tu ndiye mwamba wangu na wokovu wangu, Ngome yangu, sitatikisika sana.
3 Hata lini mtamshambulia mtu, Mpate kumwua ninyi nyote pamoja? Kama ukuta unaoinama, Kama kitalu kilicho tayari kuanguka,
4 Hufanya shauri kumwangusha tu katika cheo chake; Huufurahia uongo. Kwa kinywa chao hubariki; Kwa moyo wao hulaani.
5 Nafsi yangu, umngoje Mungu peke yake kwa kimya. Tumaini langu hutoka kwake.
6 Yeye tu ndiye mwamba wangu na wokovu wangu, Ngome yangu, sitatikisika sana.
7 Kwa Mungu wokovu wangu, Na utukufu wangu; Mwamba wa nguvu zangu, Na kimbilio langu ni kwa Mungu.
8 Enyi watu, mtumainini sikuzote, Ifunueni mioyo yenu mbele zake; Mungu ndiye kimbilio letu.
9 Hakika binadamu ni ubatili, Na wenye cheo ni uongo, Katika mizani huinuka; Wote pamoja ni hafifu kuliko ubatili.
10 Msiitumainie dhuluma, Wala msijivune kwa unyang'anyi; Mali izidipo msiiangalie sana moyoni.
11 Mara moja amenena Mungu; Mara mbili nimeyasikia haya, Ya kuwa nguvu zina Mungu,
12 Na fadhili ziko kwako, Ee Bwana; Maana ndiwe umlipaye kila mtu Sawasawa na haki yake.