Zaburi 61
1 Ee Mungu, ukisikie kilio changu, Uyasikilize maombi yangu.
2 Toka mwisho wa nchi nitakulilia nikizimia moyo, Uniongoze juu ya mwamba nisioweza kuupanda.
3 Kwa maana ulikuwa kimbilio langu, Ngome yenye nguvu adui asinipate.
4 Nitakaa katika hema yako milele, Nitaikimbilia sitara ya mbawa zako
5 Maana Wewe, Mungu, umezisikia nadhiri zangu. Umewapa urithi wao waliogopao jina lako.
6 Utaziongeza siku za mfalme, Miaka yake itakuwa kama vizazi vingi.
7 Atakaa mbele za Mungu milele, Ziagize fadhili na kweli zimhifadhi.
8 Ndivyo nitakavyoliimbia jina lako daima, Ili niondoe nadhiri zangu kila siku.