Zaburi 6
1 Bwana, usinikemee kwa hasira yako, Wala usinirudi kwa ghadhabu yako.
2 Bwana, unifadhili, maana ninanyauka; Bwana, uniponye, mifupa yangu imefadhaika.
3 Na nafsi yangu imefadhaika sana; Na Wewe, Bwana, hata lini?
4 Bwana urudi, uniopoe nafsi yangu, Uniokoe kwa ajili ya fadhili zako.
5 Maana mautini hapana kumbukumbu lako; Katika kuzimu ni nani atakayekushukuru?
6 Nimechoka kwa kuugua kwangu; Kila usiku nakieleza kitanda changu; Nalilowesha godoro langu kwa machozi yangu.
7 Jicho langu limeharibika kwa masumbufu, Na kuchakaa kwa sababu yao wanaoniudhi.
8 Ondokeni kwangu, ninyi nyote mtendao uovu; Kwa kuwa Bwana ameisikia sauti ya kilio changu.
9 Bwana ameisikia dua yangu; Bwana atayatakabali maombi yangu.
10 Adui zangu wote wataaibika na kufadhaika, Watarudi nyuma, kwa ghafula wataaibika.