«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »

Zaburi 58

1  Ni kweli, enyi wakuu, mnanena haki? Enyi wanadamu, mnahukumu kwa adili?

2  Sivyo! Mioyoni mwenu mnatenda maovu; Katika nchi mnapima udhalimu wa mikono yenu.

3  Wasio haki wamejitenga tangu kuzaliwa kwao; Tangu tumboni wamepotea, wakisema uongo.

4  Sumu yao, mfano wake ni sumu ya nyoka; Mfano wao ni fira kiziwi azibaye sikio lake.

5  Asiyeisikiliza sauti ya waganga, Ijapo wanafanya uganga kwa ustadi.

6  Ee Mungu, uyavunje meno yao vinywani mwao; Ee Bwana, uyavunje magego ya wana-simba.

7  Na watoweke kama maji yapitayo kwa kasi; Akiielekeza mishale yake, iwe imetiwa ubutu.

8  Kama konokono ayeyukaye na kutoweka, Kama mimba iliyoharibika, isiyoliona jua,

9  Kabla ya masufuria yenu kupata moto wa miiba, Ataipeperusha kama chamchela, Iliyo mibichi na iliyo moto.

10  Mwenye haki atafurahi akionapo kisasi; Ataiosha miguu yake katika damu ya wasio haki.

11  Na mwanadamu atasema, Hakika iko thawabu yake mwenye haki. Hakika yuko Mungu Anayehukumu katika dunia.

«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »
“Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi.” — 1 Wakorintho 16:23