Zaburi 54
1 Ee Mungu, kwa jina lako uniokoe, Na kwa uweza wako unifanyie hukumu.
2 Ee Mungu, uyasikie maombi yangu, Uyasikilize maneno ya kinywa changu.
3 Kwa maana wageni wamenishambulia; Watu watishao wananitafuta nafsi yangu; Hawakumweka Mungu mbele yao.
4 Tazama, Mungu ndiye anayenisaidia; Bwana ndiye anayenitegemeza nafsi yangu.
5 Atawarudishia adui zangu ubaya wao; Uwaangamize kwa uaminifu wako.
6 Kwa ukunjufu wa moyo nitakutolea dhabihu; Ee Bwana, nitalishukuru jina lako, maana ni jema.
7 Kwa kuwa limeniokoa na kila taabu; Na jicho langu limeridhika Kwa kuwatazama adui zangu.