Zaburi 50
1 Mungu, Mungu Bwana, amenena, ameiita nchi, Toka maawio ya jua hata machweo yake.
2 Tokea Sayuni, ukamilifu wa uzuri, Mungu amemulika.
3 Mungu wetu atakuja wala hatanyamaza, Moto utakula mbele zake, na tufani yavuma sana ikimzunguka pande zote.
4 Ataziita mbingu zilizo juu, Na nchi pia awahukumu watu wake.
5 Nikusanyieni wacha Mungu wangu Waliofanya agano nami kwa dhabihu.
6 Na mbingu zitatangaza haki yake, Kwa maana Mungu ndiye aliye hakimu.
7 Sikieni, enyi watu wangu, nami nitanena, Mimi nitakushuhudia, Israeli; Mimi ndimi niliye MUNGU, Mungu wako.
8 Sitakukemea kwa ajili ya dhabihu zako, Na kafara zako ziko mbele zangu daima.
9 Sitatwaa ng'ombe katika nyumba yako, Wala beberu katika mazizi yako.
10 Maana kila hayawani ni wangu, Na makundi juu ya milima elfu.
11 Nawajua ndege wote wa milima, Na wanyama wote wa mashamba ni wangu
12 Kama ningekuwa na njaa singekuambia, Maana ulimwengu ni wangu, navyo viujazavyo.
13 Je! Nile nyama ya mafahali! Au ninywe damu ya mbuzi!
14 Mtolee Mungu dhabihu za kushukuru; Mtimizie Aliye juu nadhiri zako.
15 Ukaniite siku ya mateso; Nitakuokoa, na wewe utanitukuza.
16 Bali mtu asiye haki, Mungu amwambia, Una nini wewe kuitangaza sheria yangu, Na kuliweka agano langu kinywani mwako?
17 Maana wewe umechukia maonyo, Na kuyatupa maneno yangu nyuma yako.
18 Ulipomwona mwivi ulikuwa radhi naye, Ukashirikiana na wazinzi.
19 Umekiachia kinywa chako kinene mabaya, Na ulimi wako watunga hila.
20 Umekaa na kumsengenya ndugu yako, Na mwana wa mama yako umemsingizia.
21 Ndivyo ulivyofanya, nami nikanyamaza; Ukadhani ya kuwa Mimi ni kama wewe. Walakini nitakukemea; Nitayapanga hayo mbele ya macho yako.
22 Yafahamuni hayo, Ninyi mnaomsahau Mungu, Nisije nikawararueni, Asipatikane mwenye kuwaponya.
23 Atoaye dhabihu za kushukuru, Ndiye anayenitukuza. Naye autengenezaye mwenendo wake, Nitamwonyesha wokovu wa Mungu.