Zaburi 47
1 Enyi watu wote, pigeni makofi, Mpigieni Mungu kelele kwa Sauti ya shangwe.
2 Kwa kuwa Bwana Aliye juu, mwenye kuogofya, Ndiye mfalme mkuu juu ya dunia yote.
3 Atawatiisha watu wa nchi chini yetu, Na mataifa chini ya miguu yetu.
4 Atatuchagulia urithi wetu, Fahari ya Yakobo ambaye alimpenda.
5 Mungu amepaa kwa kelele za shangwe, Bwana kwa sauti ya baragumu.
6 Mwimbieni Mungu, naam, imbeni; Mwimbieni mfalme wetu, naam, imbeni.
7 Maana Mungu ndiye mfalme wa dunia yote, Imbeni kwa akili.
8 Mungu awamiliki mataifa, Mungu ameketi katika kiti chake kitakatifu.
9 Wakuu wa watu wamekusanyika, Wawe watu wa Mungu wa Ibrahimu. Maana ngao za dunia zina Mungu, Ametukuka sana.