Zaburi 46
1 Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso.
2 Kwa hiyo hatutaogopa ijapobadilika nchi, Ijapotetemeka milima moyoni mwa bahari.
3 Maji yake yajapovuma na kuumuka, Ijapopepesuka milima kwa kiburi chake.
4 Kuna mto, vijito vyake vyaufurahisha mji wa Mungu, Patakatifu pa maskani zake Aliye juu.
5 Mungu yu katikati yake hautatetemeshwa; Mungu atausaidia asubuhi na mapema.
6 Mataifa yalighadhibika, falme zikataharuki; Alitoa sauti yake, nchi ikayeyuka.
7 Bwana wa majeshi yu pamoja nasi, Mungu wa Yakobo ni ngome yetu.
8 Njoni myatazame matendo ya Bwana, Jinsi alivyofanya ukiwa katika nchi.
9 Avikomesha vita hata mwisho wa dunia; Avunja uta, akata mkuki, achoma moto magari.
10 Acheni, mjue ya kuwa Mimi ni Mungu, Nitakuzwa katika mataifa, nitakuzwa katika nchi.
11 Bwana wa majeshi yu pamoja nasi, Mungu wa Yakobo ni ngome yetu.