Zaburi 44
1 Ee Mungu, tumesikia kwa masikio yetu Baba zetu wametuambia, Matendo uliyoyatenda siku zao, siku za kale.
2 Wewe kwa mkono wako uliwafukuza mataifa, Ukawakalisha wao. Wewe uliwatesa watu wa nchi, Ukawaeneza wao.
3 Maana si kwa upanga wao walivyoimiliki nchi, Wala si mkono wao uliowaokoa; Bali mkono wako wa kuume, naam, mkono wako, Na nuru ya uso wako, kwa kuwa uliwaridhia.
4 Ee Mungu, Wewe ndiwe mfalme wangu, Uagize mambo ya wokovu kwa Yakobo.
5 Kwa nguvu zako tutawaangusha watesi wetu; Kwa jina lako tutawakanyaga watupingao.
6 Maana sitautumainia upinde wangu, Wala upanga wangu hautaniokoa.
7 Bali Wewe ndiwe uliyetuokoa na watesi wetu; Na watuchukiao umewaaibisha.
8 Tumejisifia Mungu mchana kutwa, Na jina lako tutalishukuru milele.
9 Lakini umetutupa, umetufedhehesha, Wala hutoki na majeshi yetu.
10 Waturudisha nyuma tukampa mtesi kisogo, Na watuchukiao wanajipatia mateka.
11 Umetutoa kama kondoo tuwe chakula, Na kututawanya kati ya mataifa.
12 Wawauza watu wako bila kupata mali, Wala hukupata faida kwa thamani yao.
13 Umetufanya kuwa lawama kwa jirani zetu, Mzaha na dhihaka kwao wanaotuzunguka.
14 Umetufanya kuwa mithali kwa mataifa, Sababu ya kutikisa kichwa kwa watu wa nchi.
15 Mchana kutwa fedheha yangu i mbele yangu, Na haya ya uso wangu imenifunika,
16 Kwa sauti ya mwenye kulaumu na kukufuru, Kwa sababu ya adui na mjilipiza kisasi.
17 Haya yote yametupata, bali hatukukusahau, Wala hatukulihalifu agano lako.
18 Hatukuiacha mioyo yetu irudi nyuma, Wala hatua zetu hazikuiacha njia yako.
19 Hata utuponde katika kao la mbwa-mwitu, Na kutufunika kwa uvuli wa mauti.
20 Ikiwa tumelisahau jina la Mungu wetu, Au kumnyoshea mungu mgeni mikono yetu;
21 Je! Mungu hatalichunguza neno hilo? Maana ndiye azijuaye siri za moyo.
22 Hasha! Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa; Tunafanywa kondoo waendao kuchinjwa.
23 Amka, Bwana, mbona umelala? Ondoka, usitutupe kabisa.
24 Mbona unatuficha uso wako, Na kusahau kuonewa na kudhulumiwa kwetu?
25 Maana nafsi yetu imeinama mavumbini, Tumbo letu limegandamana na nchi.
26 Uondoke, uwe msaada wetu, Utukomboe kwa ajili ya fadhili zako.