Zaburi 41
1 Heri amkumbukaye mnyonge; Bwana atamwokoa siku ya taabu.
2 Bwana atamlinda na kumhifadhi hai, Naye atafanikiwa katika nchi; Wala usimtie katika hali wamtakiayo adui zake.
3 Bwana atamtegemeza alipo mgonjwa kitandani. Katika ugonjwa wake umemtandikia.
4 Nami nalisema, Bwana, unifadhili, Uniponye roho yangu maana nimekutenda dhambi.
5 Adui zangu wananitaja kwa maneno mabaya, Atakufa lini, jina lake likapotea?
6 Na mmoja wao akija kunitazama asema uongo, Moyo wake hujikusanyia maovu, Naye atokapo nje huyanena.
7 Wote wanaonichukia wananinong'ona, Wananiwazia mabaya.
8 Neno la kisirani limemgandama, Na iwapo amelala hatasimama tena.
9 Msiri wangu tena niliyemtumaini, Aliyekula chakula changu, Ameniinulia kisigino chake.
10 Lakini Wewe, Bwana, unifadhili, Uniinue nipate kuwalipa.
11 Kwa neno hili nimejua ya kuwa wapendezwa nami, Kwa kuwa adui yangu hasimangi kwa kunishinda.
12 Nami katika ukamilifu wangu umenitegemeza, Umeniweka mbele za uso wako milele.
13 Na atukuzwe Bwana, Mungu wa Israeli, Tangu milele hata milele. Amina na Amina.