Zaburi 35
1 Ee Bwana, utete nao wanaoteta nami, Upigane nao wanaopigana nami.
2 Uishike ngao na kigao, Usimame unisaidie.
3 Uutoe na mkuki uwapinge wanaonifuatia, Uiambie nafsi yangu, Mimi ni wokovu wako.
4 Waaibishwe, wafedheheshwe, Wanaoitafuta nafsi yangu. Warudishwe nyuma, wafadhaishwe, Wanaonizulia mabaya.
5 Wawe kama makapi mbele ya upepo, Malaika wa Bwana akiwaangusha chini.
6 Njia yao na iwe giza na utelezi, Malaika wa Bwana akiwafuatia.
7 Maana bila sababu wamenifichia wavu, Bila sababu wameichimbia shimo nafsi yangu.
8 Uharibifu na umpate kwa ghafula, Na wavu aliouficha umnase yeye mwenyewe; Kwa uharibifu aanguke ndani yake.
9 Na nafsi yangu itamfurahia Bwana, Na kuushangilia wokovu wake.
10 Mifupa yangu yote itasema, Bwana, ni nani aliye kama Wewe? Umponyaye maskini na mtu aliye hodari kumshinda yeye, Naam, maskini na mhitaji na mtu amtekaye.
11 Mashahidi wa udhalimu wanasimama, Wananiuliza mambo nisiyoyajua.
12 Wananilipa mabaya badala ya mema, Hata nafsi yangu ikaingia ukiwa.
13 Bali mimi, walipougua wao, Nguo yangu ilikuwa gunia. Nalijitesa nafsi yangu kwa kufunga; Maombi yangu yakarejea kifuani mwangu.
14 Nalijifanya kama kwamba ni rafiki au ndugu yangu, Naliinama nikilia kama aliyefiwa na mamaye.
15 Lakini nikijikwaa hufurahi na kukusanyana, Walinikusanyikia watu ovyo nisiowajua, Wananipapura wala hawakomi.
16 Kama wenye mzaha wakikufuru karamuni Wananisagia meno.
17 Bwana, hata lini utatazama? Uiokoe nafsi yangu na maharabu yao, Na mpenzi wangu na wana-simba.
18 Nitakushukuru katika kusanyiko kubwa; Nitakusifu kati ya watu wengi.
19 Walio adui zangu bure wasinisimange, Wanaonichukia bila sababu wasining'ong'e.
20 Maana hawasemi maneno ya amani, Na juu ya watulivu wa nchi huwaza hila.
21 Nao wananifumbulia vinywa vyao, Husema, Ewe! Ewe! Jicho letu limeona.
22 Wewe, Bwana, umeona, usinyamaze; Ee Bwana, usiwe mbali nami.
23 Uamke, uwe macho ili kunipatia hukumu Kwa ajili ya madai yangu, Mungu wangu na Bwana wangu.
24 Unihukumu kwa haki yako, Ee Bwana, Mungu wangu, Wala wasinisimangize.
25 Wasiseme moyoni, Haya! Ndivyo tutakavyo; Wasiseme, Tumemmeza.
26 Waaibishwe, wafedheheshwe pamoja, Wanaoifurahia hali yangu mbaya. Wavikwe aibu na fedheha, Wanaojikuza juu yangu.
27 Washangilie na kufurahi, Wapendezwao na haki yangu. Naam, waseme daima, Atukuzwe Bwana, Apendezwaye na amani ya mtumishi wake.
28 Na ulimi wangu utanena haki yako, Na sifa zako mchana kutwa.