«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »

Zaburi 32

1  Heri aliyesamehewa dhambi, Na kusitiriwa makosa yake.

2  Heri Bwana asiyemhesabia upotovu, Ambaye rohoni mwake hamna hila.

3  Niliponyamaza mifupa yangu ilichakaa Kwa kuugua kwangu mchana kutwa.

4  Kwa maana mchana na usiku Mkono wako ulinilemea. Jasho langu likakauka hata nikawa Kama nchi kavu wakati wa kaskazi.

5  Nalikujulisha dhambi yangu, Wala sikuuficha upotovu wangu. Nalisema, Nitayakiri maasi yangu kwa Bwana, Nawe ukanisamehe upotovu wa dhambi yangu.

6  Kwa hiyo kila mtu mtauwa Akuombe wakati unapopatikana. Hakika maji makuu yafurikapo, Hayatamfikia yeye.

7  Ndiwe sitara yangu, utanihifadhi na mateso, Utanizungusha nyimbo za wokovu.

8  Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea; Nitakushauri, jicho langu likikutazama.

9  Msiwe kama farasi wala nyumbu, Walio hawana akili. Kwa matandiko ya lijamu na hatamu Sharti kuwazuia hao, au hawatakukaribia.

10  Naye mtu mwovu ana mapigo mengi, Bali amtumainiye Bwana fadhili zitamzunguka.

11  Mfurahieni Bwana; Shangilieni, enyi wenye haki Pigeni vigelegele vya furaha; Ninyi nyote mlio wanyofu wa moyo.

«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »
“Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi.” — 1 Wakorintho 16:23