«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »

Zaburi 30

1  Ee Bwana, nitakutukuza kwa maana umeniinua, Wala hukuwafurahisha adui zangu juu yangu.

2  Ee Bwana, Mungu wangu, Nalikulilia ukaniponya.

3  Umeniinua nafsi yangu, Ee Bwana, kutoka kuzimu. Umenihuisha na kunitoa Miongoni mwao washukao shimoni.

4  Mwimbieni Bwana zaburi, Enyi watauwa wake. Na kufanya shukrani. Kwa kumbukumbu la utakatifu wake.

5  Maana ghadhabu zake ni za kitambo kidogo, Katika radhi yake mna uhai. Huenda kilio huja kukaa usiku, Lakini asubuhi huwa furaha.

6  Nami nilipofanikiwa nalisema, Sitaondoshwa milele.

7  Bwana, kwa radhi yako Wewe uliuimarisha mlima wangu. Uliuficha uso wako, Nami nikafadhaika.

8  Ee Bwana, nalikulilia Wewe, Naam, kwa Bwana naliomba dua.

9  Mna faida gani katika damu yangu Nishukapo shimoni? Mavumbi yatakusifu? Yataitangaza kweli yako?

10  Ee Bwana, usikie, unirehemu, Bwana, uwe msaidizi wangu.

11  Uligeuza matanga yangu kuwa machezo; Ulinivua gunia, ukanivika furaha.

12  Ili utukufu wangu ukusifu, Wala usinyamaze. Ee Bwana, Mungu wangu, Nitakushukuru milele.

«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »
“Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi.” — 1 Wakorintho 16:23