«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »

Zaburi 29

1  Mpeni Bwana, enyi wana wa Mungu, Mpeni Bwana utukufu na nguvu;

2  Mpeni Bwana utukufu wa jina lake; Mwabuduni Bwana kwa uzuri wa utakatifu.

3  Sauti ya Bwana i juu ya maji; Mungu wa utukufu alipiga radi; Bwana yu juu ya maji mengi.

4  Sauti ya Bwana ina nguvu; Sauti ya Bwana ina adhama;

5  Sauti ya Bwana yaivunja mierezi; Naam, Bwana aivunja-vunja mierezi ya Lebanoni;

6  Airusha-rusha kama ndama wa ng'ombe; Lebanoni na Sirioni kama mwana-nyati.

7  Sauti ya Bwana yaipasua miali ya moto;

8  Sauti ya Bwana yalitetemesha jangwa; Bwana alitetemesha jangwa la Kadeshi.

9  Sauti ya Bwana yawazalisha ayala, Na kuifichua misitu; Na ndani ya hekalu lake Wanasema wote, Utukufu.

10  Bwana aliketi juu ya Gharika; Naam, Bwana ameketi hali ya mfalme milele.

11  Bwana atawapa watu wake nguvu; Bwana atawabariki watu wake kwa amani.

«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »
“Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi.” — 1 Wakorintho 16:23