Zaburi 28
1 Ee Bwana, nitakuita Wewe, mwamba wangu, Usiwe kwangu kama kiziwi. Nisije nikafanana nao washukao shimoni, Ikiwa umeninyamalia.
2 Uisikie sauti ya dua yangu nikuombapo, Nikipainulia patakatifu pako mikono yangu.
3 Usinikokote pamoja na wasio haki, Wala pamoja na watenda maovu. Wawaambiao jirani zao maneno ya amani, Lakini mioyoni mwao mna madhara.
4 Uwape sawasawa na vitendo vyao, Na kwa kadiri ya ubaya wa kufanya kwao, Uwape sawasawa na kazi ya mikono yao, Uwalipe stahili zao.
5 Maana hawazifahamu kazi za Bwana, Wala matendo ya mikono yake. Atawavunja wala hatawajenga;
6 Na ahimidiwe Bwana. Maana ameisikia sauti ya dua yangu;
7 Bwana ni nguvu zangu na ngao yangu. Moyo wangu umemtumaini, Nami nimesaidiwa; Basi, moyo wangu unashangilia, Na kwa wimbo wangu nitamshukuru.
8 Bwana ni nguvu za watu wake, Naye ni ngome ya wokovu kwa masihi
9 Uwaokoe watu wako, uubariki urithi wako, Uwachunge, uwachukue milele.