Zaburi 25
1 Ee Bwana, nakuinulia nafsi yangu,
2 Ee Mungu wangu, Nimekutumaini Wewe, nisiaibike, Adui zangu wasifurahi kwa kunishinda.
3 Naam, wakungojao hawataaibika hata mmoja; Wataaibika watendao uhaini bila sababu.
4 Ee Bwana, unijulishe njia zako, Unifundishe mapito yako,
5 Uniongoze katika kweli yako, Na kunifundisha. Maana Wewe ndiwe Mungu wa wokovu wangu, Nakungoja Wewe mchana kutwa.
6 Ee Bwana, kumbuka rehema zako na fadhili zako, Maana zimekuwako tokea zamani.
7 Usiyakumbuke makosa ya ujana wangu, Wala maasi yangu. Unikumbuke kwa kadiri ya fadhili zako, Ee Bwana kwa ajili ya wema wako.
8 Bwana yu mwema, mwenye adili, Kwa hiyo atawafundisha wenye dhambi njia.
9 Wenye upole atawaongoza katika hukumu, Wenye upole atawafundisha njia yake.
10 Njia zote za Bwana ni fadhili na kweli, Kwao walishikao agano lake na shuhuda zake.
11 Ee Bwana, kwa ajili ya jina lako, Unisamehe uovu wangu, maana ni mwingi.
12 Ni nani amchaye Bwana? Atamfundisha katika njia anayoichagua.
13 Nafsi yake itakaa hali ya kufanikiwa; Wazao wake watairithi nchi.
14 Siri ya Bwana iko kwao wamchao, Naye atawajulisha agano lake.
15 Macho yangu humwelekea Bwana daima, Naye atanitoa miguu yangu katika wavu.
16 Uniangalie na kunifadhili, Maana mimi ni mkiwa na mteswa.
17 Katika shida za moyo wangu unifanyie nafasi, Na kunitoa katika dhiki zangu.
18 Utazame teso langu na taabu yangu; Unisamehe dhambi zangu zote.
19 Uwatazame adui zangu, maana ni wengi, Wananichukia kwa machukio ya ukali.
20 Unilinde nafsi yangu na kuniponya, Nisiaibike, maana nakukimbilia Wewe.
21 Ukamilifu na unyofu zinihifadhi, Maana nakungoja Wewe.
22 Ee Mungu, umkomboe Israeli, Katika taabu zake zote.