«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »

Zaburi 17

1  Ee Bwana, usikie haki, ukisikilize kilio changu, Utege sikio lako kwa maombi yangu, Yasiyotoka katika midomo ya hila.

2  Hukumu yangu na itoke kwako, Macho yako na yatazame mambo ya adili.

3  Umenijaribu moyo wangu, umenijilia usiku, Umenihakikisha usione neno; Nimenuia kinywa changu kisikose,

4  Mintarafu matendo ya wanadamu; Kwa neno la midomo yako Nimejiepusha na njia za wenye jeuri.

5  Nyayo zangu zimeshikamana na njia zako, Hatua zangu hazikuondoshwa.

6  Ee Mungu, nimekuita kwa maana utaitika, Utege sikio lako ulisikie neno langu.

7  Dhihirisha fadhili zako za ajabu Wewe uwaokoaye wanaokukimbilia; Kwa mkono wako wa kuume Uwaokoe nao wanaowaondokea.

8  Unilinde kama mboni ya jicho, Unifiche chini ya uvuli wa mbawa zako;

9  Wasinione wasio haki wanaonionea, Adui za roho yangu wanaonizunguka.

10  Wameukaza moyo wako, Kwa vinywa vyao hutoa majivuno.

11  Sasa wametuzunguka hatua zetu, Na kuyakaza macho yao watuangushe chini.

12  Kama mfano wa simba atakaye kurarua, Kama mwana-simba aoteaye katika maoteo yake.

13  Ee Bwana, usimame, umkabili, umwinamishe, Kwa upanga wako uniokoe nafsi na mtu mbaya.

14  Ee Bwana, kwa mkono wako uniokoe na watu, Watu wa dunia hii ambao fungu lao li katika maisha haya. Matumbo yao wayajaza kwa hazina yako, Hushiba wana, huwaachia watoto wao akiba zao,

15  Bali mimi nikutazame uso wako katika haki, Niamkapo nishibishwe kwa sura yako.

«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »
“Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi.” — 1 Wakorintho 16:23