Zaburi 15
1 Bwana, ni nani atakayekaa Katika hema yako? Ni nani atakayefanya maskani yake Katika kilima chako kitakatifu?
2 Ni mtu aendaye kwa ukamilifu, Na kutenda haki. Asemaye kweli kwa moyo wake,
3 Asiyesingizia kwa ulimi wake. Wala hakumtenda mwenziwe mabaya, Wala hakumsengenya jirani yake.
4 Machoni pake mtu asiyefaa hudharauliwa, Bali huwaheshimu wamchao Bwana Ingawa ameapa kwa hasara yake, Hayabadili maneno yake.
5 Hakutoa fedha yake apate kula riba, Hakutwaa rushwa amwangamize asiye na hatia. Mtu atendaye mambo hayo Hataondoshwa milele.