Zaburi 146
1 Haleluya.
2 Nitamsifu Bwana muda ninaoishi, Nitamwimbia Mungu wangu ningali ni hai.
3 Msiwatumainie wakuu, Wala binadamu ambaye hakuna wokovu kwake.
4 Pumzi yake hutoka, huurudia udongo wake, Siku hiyo mawazo yake yapotea.
5 Heri ambaye Mungu wa Yakobo ni msaada wake, Na tumaini lake ni kwa Bwana, Mungu wake,
6 Aliyezifanya mbingu na nchi, Bahari na vitu vyote vilivyomo. Huishika kweli milele,
7 Huwafanyia hukumu walioonewa, Huwapa wenye njaa chakula; Bwana hufungua waliofungwa;
8 Bwana huwafumbua macho waliopofuka; Bwana huwainua walioinama; Bwana huwapenda wenye haki;
9 Bwana huwahifadhi wageni; Huwategemeza yatima na mjane; Bali njia ya wasio haki huipotosha.
10 Bwana atamiliki milele, Mungu wako, Ee Sayuni, kizazi hata kizazi. Haleluya.