«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »

Zaburi 143

1  Ee Bwana, uisikie sala yangu, uzisikilize dua zangu, Kwa uaminifu wako unijibu kwa haki yako.

2  Wala usimhukumu mtumishi wako, Maana kwako hakuna aliye hai mwenye haki.

3  Maana adui ameifuatia nafsi yangu, Ameutupa chini uzima wangu. Amenikalisha mahali penye giza, Kama watu waliokufa zamani.

4  Na roho yangu imezimia ndani yangu, Moyo wangu ndani yangu umesituka.

5  Nimezikumbuka siku za kale, Nimeyatafakari matendo yako yote, Naziwaza kazi za mikono yako.

6  Nakunyoshea mikono yangu; Nafsi yangu inakuonea kiu kama nchi kame.

7  Ee Bwana, unijibu hima, roho yangu imelegea; Usinifiche uso wako, Nisifanane nao washukao shimoni

8  Unifanye kusikia fadhili zako asubuhi, Kwa maana nimekutumaini Wewe. Unijulishe njia nitakayoiendea, Kwa maana nakuinulia nafsi yangu.

9  Ee Bwana, uniponye na adui zangu; Nimekukimbilia Wewe, unifiche.

10  Unifundishe kuyatenda mapenzi yako, Kwa maana ndiwe Mungu wangu; Roho yako mwema aniongoze kwenye nchi sawa,

11  Ee Bwana, unihuishe kwa ajili ya jina lako, Kwa haki yako unitoe roho yangu taabuni;

12  Kwa fadhili zako utawakatilia mbali adui zangu; Na kuwaangamiza wote wanitesao nafsi, Kwa maana mimi ni mtumishi wako.

«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »
“Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi.” — 1 Wakorintho 16:23