Zaburi 14
1 Mpumbavu amesema moyoni, Hakuna Mungu; Wameharibu matendo yao na kuyafanya chukizo, Hakuna atendaye mema.
2 Toka mbinguni Bwana aliwachungulia wanadamu, Aone kama yuko mtu mwenye akili, Amtafutaye Mungu.
3 Wote wamepotoka, wameoza wote pamoja, Hakuna atendaye mema, La! Hata mmoja.
4 Je! Wote wafanyao maovu hawajui? Walao watu wangu kama walavyo mkate, Hawamwiti Bwana.
5 Hapo ndipo walipoingiwa na hofu nyingi, Maana Mungu yupo pamoja na kizazi cha haki.
6 Mnalitia aibu shauri la mtu mnyonge, Bali Bwana ndiye aliye kimbilio lake.
7 Laiti wokovu wa Israeli utoke katika Sayuni! Bwana awarudishapo wafungwa wa watu wake; Yakobo atashangilia, Israeli atafurahi.