Zaburi 138
1 Nitakushukuru kwa moyo wangu wote, Mbele ya miungu nitakuimbia zaburi.
2 Nitasujudu nikilikabili hekalu lako takatifu, Nitalishukuru jina lako, Kwa ajili ya fadhili zako na uaminifu wako, Kwa maana umeikuza ahadi yako, Kuliko jina lako lote.
3 Siku ile niliyokuita uliniitikia, Ukanifariji nafsi kwa kunitia nguvu.
4 Ee Bwana, wafalme wote wa dunia watakushukuru, Watakapoyasikia maneno ya kinywa chako.
5 Naam, wataziimba njia za Bwana, Kwa maana utukufu wa Bwana ni mkuu.
6 Ingawa Bwana yuko juu, amwona mnyenyekevu, Naye amjua mwenye kujivuna tokea mbali.
7 Nijapokwenda kati ya shida utanihuisha, Utanyosha mkono juu ya hasira ya adui zangu, Na mkono wako wa kuume utaniokoa.
8 Bwana atanitimilizia mambo yangu; Ee Bwana, fadhili zako ni za milele; Usiziache kazi za mikono yako.