Zaburi 12
1 Bwana, uokoe, maana mcha Mungu amekoma, Maana waaminifu wametoweka katika wanadamu.
2 Husemezana yasiyofaa kila mtu na mwenziwe, Wenye midomo ya kujipendekeza; Husemezana kwa mioyo ya unafiki;
3 Bwana ataikata midomo yote ya kujipendekeza, Nao ulimi unenao maneno ya kiburi;
4 Waliosema, Kwa ndimi zetu tutashinda; Midomo yetu ni yetu wenyewe, Ni nani aliye bwana juu yetu?
5 Kwa ajili ya kuonewa kwao wanyonge, Kwa ajili ya kuugua kwao wahitaji, Sasa nitasimama, asema Bwana, Nitamweka salama yeye wanayemfyonya.
6 Maneno ya Bwana ni maneno safi, Ni fedha iliyojaribiwa kalibuni juu ya nchi; Iliyosafishwa mara saba.
7 Wewe, Bwana, ndiwe utakayetuhifadhi, Utatulinda na kizazi hiki milele.
8 Wasio haki hutembea pande zote, Ufisadi ukitukuka kati ya wanadamu.