Zaburi 119
1 Heri walio kamili njia zao, Waendao katika sheria ya Bwana.
2 Heri wazitiio shuhuda zake, Wamtafutao kwa moyo wote.
3 Naam, hawakutenda ubatili, Wamekwenda katika njia zake.
4 Wewe umetuamuru mausia yako, Ili sisi tuyatii sana.
5 Ningependa njia zangu ziwe thabiti, Nizitii amri zako.
6 Ndipo mimi sitaaibika, Nikiyaangalia maagizo yako yote.
7 Nitakushukuru kwa unyofu wa moyo, Nikiisha kujifunza hukumu za haki yako
8 Nitazitii amri zako, Usiniache kabisa
9 Jinsi gani kijana aisafishe njia yake? Kwa kutii, akilifuata neno lako.
10 Kwa moyo wangu wote nimekutafuta, Usiniache nipotee mbali na maagizo yako.
11 Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi.
12 Ee Bwana, umehimidiwa, Unifundishe amri zako.
13 Kwa midomo yangu nimezisimulia Hukumu zote za kinywa chako.
14 Nimeifurahia njia ya shuhuda zako Kana kwamba ni mali mengi.
15 Nitayatafakari mausia yako, Nami nitaziangalia njia zako.
16 Nitajifurahisha sana kwa amri zako, Sitalisahau neno lako.
17 Umtendee mtumishi wako ukarimu, Nipate kuishi, nami nitalitii neno lako.
18 Unifumbue macho yangu niyatazame Maajabu yatokayo katika sheria yako.
19 Mimi ni mgeni katika nchi, Usinifiche maagizo yako.
20 Roho yangu imepondeka kwa kutamani Hukumu zako kila wakati.
21 Umewakemea wenye kiburi, Wamelaaniwa waendao mbali na maagizo yako.
22 Uniondolee laumu na dharau, Kwa maana nimezishika shuhuda zako.
23 Wakuu nao waliketi wakaninena, Lakini mtumishi wako atazitafakari amri zako.
24 Shuhuda zako nazo ndizo furaha yangu, Na washauri wangu.
25 Nafsi yangu imeambatana na mavumbi, Unihuishe sawasawa na neno lako.
26 Nalizisimulia njia zangu ukanijibu, Unifundishe amri zako.
27 Unifahamishe njia ya mausia yako, Nami nitayatafakari maajabu yako.
28 Nafsi yangu imeyeyuka kwa uzito, Unitie nguvu sawasawa na neno lako.
29 Uniondolee njia ya uongo, Unineemeshe kwa sheria yako.
30 Nimeichagua njia ya uaminifu, Na kuziweka hukumu zako mbele yangu.
31 Nimeambatana na shuhuda zako, Ee Bwana, usiniaibishe.
32 Nitakwenda mbio katika njia ya maagizo yako, Utakaponikunjua moyo wangu.
33 Ee Bwana, unifundishe njia ya amri zako, Nami nitaishika hata mwisho.
34 Unifahamishe nami nitaishika sheria yako, Naam, nitaitii kwa moyo wangu wote.
35 Uniendeshe katika mapito ya maagizo yako, Kwa maana nimependezwa nayo.
36 Unielekeze moyo wangu na shuhuda zako, Wala usiielekee tamaa.
37 Unigeuze macho yangu nisitazame visivyofaa, Unihuishe katika njia yako.
38 Umthibitishie mtumishi wako ahadi yako, Inayohusu kicho chako.
39 Uniondolee laumu niiogopayo, Maana hukumu zako ni njema.
40 Tazama, nimeyatamani mausia yako, Unihuishe kwa haki yako.
41 Ee Bwana, fadhili zako zinifikie na mimi, Naam, wokovu wako sawasawa na ahadi yako.
42 Nami nitamjibu neno anilaumuye, Kwa maana nalitumainia neno lako.
43 Usiliondoe neno la kweli kinywani mwangu kamwe, Maana nimezingojea hukumu zako.
44 Nami nitaitii sheria yako daima, Naam, milele na milele.
45 Nami nitakwenda panapo nafasi, Kwa kuwa nimejifunza mausia yako.
46 Nitazinena shuhuda zako mbele ya wafalme, Wala sitaona aibu.
47 Nami nitajifurahisha sana kwa maagizo yako, Ambayo nimeyapenda.
48 Na mikono yangu nitayainulia maagizo yako niliyoyapenda, Nami nitazitafakari amri zako.
49 Likumbuke neno ulilomwambia mtumishi wako, Kwa sababu umenitumainisha.
50 Hii ndiyo faraja yangu katika taabu yangu, Ya kwamba ahadi yako imenihuisha.
51 Wenye kiburi wamenidharau mno, Sikujiepusha na sheria zako.
52 Nimezikumbuka hukumu zako za kale, Ee Bwana, nikajifariji.
53 Ghadhabu imenishika kwa sababu ya wasio haki, Waiachao sheria yako.
54 Amri zako zimekuwa nyimbo zangu, Katika nyumba ya ugeni wangu.
55 Wakati wa usiku nimelikumbuka jina lako, Ee Bwana, nikaitii sheria yako.
56 Hayo ndiyo niliyokuwa nayo, Kwa sababu nimeyashika mausia yako.
57 Bwana ndiye aliye fungu langu, Nimesema kwamba nitayatii maneno yake.
58 Nimekuomba radhi kwa moyo wangu wote, Unifadhili sawasawa na ahadi yako.
59 Nalizitafakari njia zangu, Na miguu yangu nalizielekezea shuhuda zako.
60 Nalifanya haraka wala sikukawia, Kuyatii maagizo yako.
61 Kamba za wasio haki zimenifunga, Sikuisahau sheria yako.
62 Katikati ya usiku nitaamka nikushukuru, Kwa sababu ya hukumu zako za haki.
63 Mimi ni mwenzao watu wote wakuchao, Na wale wayatiio mausia yako.
64 Bwana, dunia imejaa fadhili zako, Unifundishe amri zako.
65 Umemtendea mema mtumishi wako, Ee Bwana, sawasawa na neno lako.
66 Unifundishe akili na maarifa, Maana nimeyaamini maagizo yako.
67 Kabla sijateswa mimi nalipotea, Lakini sasa nimelitii neno lako.
68 Wewe U mwema na mtenda mema, Unifundishe amri zako.
69 Wenye kiburi wamenizulia uongo, Kwa moyo wangu wote nitayashika mausia yako.
70 Mioyo yao imenenepa kama shahamu, Mimi nimeifurahia sheria yako.
71 Ilikuwa vema kwangu kuwa naliteswa, Nipate kujifunza amri zako.
72 Sheria ya kinywa chako ni njema kwangu, Kuliko maelfu ya dhahabu na fedha.
73 Mikono yako ilinifanya ikanitengeneza, Unifahamishe nikajifunze maagizo yako.
74 Wakuchao na wanione na kufurahi, Kwa sababu nimelingojea neno lako.
75 Najua ya kuwa hukumu zako ni za haki, Ee Bwana, na kwa uaminifu umenitesa.
76 Nakuomba, fadhili zako ziwe faraja kwangu, Sawasawa na ahadi yako kwa mtumishi wako.
77 Rehema zako zinijie nipate kuishi, Maana sheria yako ni furaha yangu.
78 Wenye kiburi waaibike, maana wamenidhulumu kwa uongo, Mimi nitayatafakari mausia yako.
79 Wakuchao na wanirudie, Nao watazijua shuhuda zako.
80 Moyo wangu na uwe mkamilifu katika amri zako, Nisije mimi nikaaibika.
81 Nafsi yangu imefifia kwa kuutamani wokovu wako, Nimelingojea neno lako.
82 Macho yangu yamefifia kwa kuitazamia ahadi yako, Nisemapo, Lini utakaponifariji?
83 Maana nimekuwa kama kiriba katika moshi, Sikuzisahau amri zako.
84 Siku za mtumishi wako ni ngapi, Lini utakapowahukumu wale wanaonifuatia?
85 Wenye kiburi wamenichimbia mashimo, Ambao hawaifuati sheria yako.
86 Maagizo yako yote ni amini, Wananifuatia bure, unisaidie.
87 Walikuwa karibu na kunikomesha katika nchi, Lakini sikuyaacha mausia yako.
88 Unihuishe kwa fadhili zako, Nami nitazishika shuhuda za kinywa chako.
89 Ee Bwana, neno lako lasimama Imara mbinguni hata milele.
90 Uaminifu wako upo kizazi baada ya kizazi, Umeiweka nchi, nayo inakaa.
91 Kwa hukumu zako vimesimama imara hata leo, Maana vitu vyote ni watumishi wako.
92 Kama sheria yako isingalikuwa furaha yangu, Hapo ningalipotea katika taabu zangu.
93 Hata milele sitayasahau maagizo yako, Maana kwa hayo umenihuisha.
94 Mimi ni wako, uniokoe, Kwa maana nimejifunza mausia yako.
95 Wasio haki wameniotea ili kunipoteza, Nitazitafakari shuhuda zako.
96 Nimeona ukamilifu wote kuwa na mwisho, Bali agizo lako ni pana mno.
97 Sheria yako naipenda mno ajabu, Ndiyo kutafakari kwangu mchana kutwa.
98 Maagizo yako hunitia hekima kuliko adui zangu, Kwa maana ninayo sikuzote.
99 Ninazo akili kuliko wakufunzi wangu wote, Maana shuhuda zako ndizo nizifikirizo.
100 Ninao ufahamu kuliko wazee, Kwa kuwa nimeyashika mausia yako.
101 Nimeiepusha miguu yangu na kila njia mbaya, Ili nilitii neno lako.
102 Sikujiepusha na hukumu zako, Maana Wewe mwenyewe umenifundisha.
103 Mausia yako ni matamu sana kwangu, Kupita asali kinywani mwangu.
104 Kwa mausia yako najipatia ufahamu, Ndiyo maana naichukia kila njia ya uongo.
105 Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu.
106 Nimeapa nami nitaifikiliza, Kuzishika hukumu za haki yako.
107 Nimeteswa mno; Ee Bwana, unihuishe sawasawa na neno lako.
108 Ee Bwana, uziridhie sadaka za kinywa changu, Na kunifundisha hukumu zako.
109 Nafsi yangu imo mkononi mwangu daima, Lakini sheria yako sikuisahau.
110 Watendao uovu wamenitegea mtego, Lakini sikuikosa njia ya mausia yako.
111 Shuhuda zako nimezifanya urithi wa milele, Maana ndizo changamko la moyo wangu.
112 Nimeuelekeza moyo wangu nizitende amri zako, Daima, naam, hata milele.
113 Watu wa kusita-sita nawachukia, Lakini sheria yako naipenda.
114 Ndiwe sitara yangu na ngao yangu, Neno lako nimelingojea.
115 Enyi watenda mabaya, ondokeni kwangu, Niyashike maagizo ya Mungu wangu.
116 Unitegemeze sawasawa na ahadi yako, nikaishi, Wala usiniache niyaaibikie matumaini yangu.
117 Unisaidie nami nitakuwa salama, Nami nitaziangalia amri zako daima.
118 Umewakataa wote wazikosao amri zako, Kwa maana hila zao ni uongo.
119 Wabaya wa nchi pia umewaondoa kama takataka, Ndiyo maana nimezipenda shuhuda zako.
120 Mwili wangu unatetemeka kwa kukucha Wewe, Nami ninaziogopa hukumu zako.
121 Nimefanya hukumu na haki, Usiniache mikononi mwao wanaonionea.
122 Uwe mdhamini wa mtumishi wako, apate mema, Wenye kiburi wasinionee.
123 Macho yangu yamefifia kwa kuutamani wokovu wako, Na ahadi ya haki yako.
124 Kama zilivyo rehema zako umtendee mtumishi wako, Na amri zako unifundishe.
125 Mimi ni mtumishi wako, unifahamishe, Nipate kuzijua shuhuda zako.
126 Wakati umewadia Bwana atende kazi; Kwa kuwa wameitangua sheria yako.
127 Ndiyo maana nimeyapenda maagizo yako, Kuliko dhahabu, naam, dhahabu iliyo safi.
128 Maana nayaona mausia yako yote kuwa ya adili, Kila njia ya uongo naichukia.
129 Shuhuda zako ni za ajabu, Ndiyo maana roho yangu imezishika.
130 Kufafanusha maneno yako kwatia nuru, Na kumfahamisha mjinga.
131 Nalifunua kinywa changu nikatweta, Maana naliyatamani maagizo yako.
132 Unigeukie, unirehemu mimi, Kama iwahusuvyo walipendao jina lako.
133 Uzielekeze hatua zangu kwa neno lako, Uovu usije ukanimiliki.
134 Unikomboe na dhuluma ya mwanadamu, Nipate kuyashika mausia yako.
135 Umwangazie mtumishi wako uso wako, Na kunifundisha amri zako.
136 Macho yangu yachuruzika mito ya maji, Kwa sababu hawaitii sheria yako.
137 Ee Bwana, Wewe ndiwe mwenye haki, Na hukumu zako ni za adili.
138 Umeziagiza shuhuda zako kwa haki, Na kwa uaminifu mwingi.
139 Juhudi yangu imeniangamiza, Maana watesi wangu wameyasahau maneno yako.
140 Neno lako limesafika sana, Kwa hiyo mtumishi wako amelipenda.
141 Mimi ni mdogo, nadharauliwa, Lakini siyasahau mausia yako.
142 Haki yako ni haki ya milele, Na sheria yako ni kweli.
143 Taabu na dhiki zimenipata, Maagizo yako ni furaha yangu.
144 Haki ya shuhuda zako ni ya milele, Unifahamishe, nami nitaishi.
145 Nimeita kwa moyo wangu wote; Ee Bwana, uitike; Nitazishika amri zako.
146 Nimekuita Wewe, uniokoe, Nami nitazishika shuhuda zako.
147 Kutangulia mapambazuko naliomba msaada, Naliyangojea maneno yako kwa tumaini.
148 Macho yangu yalitangulia makesha ya usiku, Ili kuitafakari ahadi yako.
149 Uisikie sauti yangu sawasawa na fadhili zako, Ee Bwana, unihuishe sawasawa na hukumu yako.
150 Wanakaribia wanaonifuatia kwa chuki, Wamekwenda mbali na sheria yako.
151 Ee Bwana, Wewe U karibu, Na maagizo yako yote ni kweli.
152 Tokea zamani nimejua kwa shuhuda zako, Ya kuwa umeziweka zikae milele.
153 Uyaangalie mateso yangu, uniokoe, Maana sikuisahau sheria yako.
154 Unitetee na kunikomboa, Unihuishe sawasawa na ahadi yako.
155 Wokovu u mbali na wasio haki, Kwa maana hawajifunzi amri zako.
156 Ee Bwana, rehema zako ni nyingi, Unihuishe sawasawa na hukumu zako.
157 Wanaonifuatia na watesi wangu ni wengi, Lakini sikujiepusha na shuhuda zako.
158 Nimewaona watendao uhaini nikachukizwa, Kwa sababu hawakulitii neno lako.
159 Uangalie niyapendavyo mausia yako, Ee Bwana, unihuishe sawasawa na fadhili zako.
160 Jumla ya neno lako ni kweli, Na kila hukumu ya haki yako ni ya milele.
161 Wakuu wameniudhi bure, Ila moyo wangu unayahofia maneno yako.
162 Naifurahia ahadi yako, Kama apataye mateka mengi.
163 Nimeuchukia uongo, umenikirihi, Sheria yako nimeipenda.
164 Mara saba kila siku nakusifu, Kwa sababu ya hukumu za haki yako.
165 Wana amani nyingi waipendao sheria yako, Wala hawana la kuwakwaza.
166 Ee Bwana, nimeungojea wokovu wako, Na maagizo yako nimeyatenda.
167 Nafsi yangu imezishika shuhuda zako, Nami nazipenda mno.
168 Nimeyashika mausia yako na shuhuda zako, Maana njia zangu zote zi mbele zako.
169 Ee Bwana, kilio changu na kikukaribie, Unifahamishe sawasawa na neno lako.
170 Dua yangu na ifike mbele zako, Uniponye sawasawa na ahadi yako.
171 Midomo yangu na itoe sifa, Kwa kuwa unanifundisha mausia yako.
172 Ulimi wangu na uiimbe ahadi yako, Maana maagizo yako yote ni ya haki.
173 Mkono wako na uwe tayari kunisaidia, Maana nimeyachagua mausia yako.
174 Ee Bwana, nimeutamani wokovu wako, Na sheria yako ndiyo furaha yangu.
175 Nafsi yangu na iishi, ipate kukusifu, Na hukumu zako zinisaidie.
176 Nimetanga-tanga kama kondoo aliyepotea; Umtafute mtumishi wako; Kwa maana sikuyasahau maagizo yako.