Zaburi 113
1 Haleluya. Enyi watumishi wa Bwana, sifuni, Lisifuni jina la Bwana.
2 Jina la Bwana lihimidiwe Tangu leo na hata milele.
3 Toka maawio ya jua hata machweo yake Jina la Bwana husifiwa.
4 Bwana ni mkuu juu ya mataifa yote, Na utukufu wake ni juu ya mbingu.
5 Ni nani aliye mfano wa Bwana, Mungu wetu aketiye juu;
6 Anyenyekeaye kutazama, Mbinguni na duniani?
7 Humwinua mnyonge kutoka mavumbini, Na kumpandisha maskini kutoka jaani.
8 Amketishe pamoja na wakuu, Pamoja na wakuu wa watu wake.
9 Huweka nyumbani mwanamke aliye tasa, Awe mama ya watoto mwenye furaha.