Zaburi 110
1 Neno la Bwana kwa Bwana wangu, Uketi mkono wangu wa kuume, Hata niwafanyapo adui zako Kuwa chini ya miguu yako.
2 Bwana atainyosha toka Sayuni Fimbo ya nguvu zako. Uwe na enzi kati ya adui zako;
3 Watu wako wanajitoa kwa hiari, Siku ya uwezo wako; Kwa uzuri wa utakatifu, Tokea tumbo la asubuhi, Unao umande wa ujana wako.
4 Bwana ameapa, Wala hataghairi, Ndiwe kuhani hata milele, Kwa mfano wa Melkizedeki.
5 Bwana yu mkono wako wa kuume; Ataseta wafalme, Siku ya ghadhabu yake.
6 Atahukumu kati ya mataifa, Ataijaza nchi mizoga; Ataseta kichwa katika nchi nyingi.
7 Atakunywa maji ya mto njiani; Kwa hiyo atakiinua kichwa chake.