Zaburi 109
1 Ee Mungu wa sifa zangu, usinyamaze,
2 Kwa maana wamenifumbulia kinywa; Kinywa cha mtu asiye haki, cha hila, Wamesema nami kwa ulimi wa uongo.
3 Naam, kwa maneno ya chuki wamenizunguka, Wamepigana nami bure.
4 Badala ya upendo wangu wao hunishitaki, Ijapokuwa naliwaombea.
5 Wamenichukuza mabaya badala ya mema, Na chuki badala ya upendo wangu.
6 Uweke mtu mkorofi juu yake, Mshitaki asimame mkono wake wa kuume.
7 Katika kuhukumiwa ataonekana hana haki, Na sala yake itadhaniwa kuwa ni dhambi.
8 Siku zake na ziwe chache, Usimamizi wake na atwae mtu mwingine.
9 Wanawe na wawe yatima, Na mkewe na awe mjane.
10 Kutanga na watange wanawe na kuomba, Watafute chakula mbali na mahame yao.
11 Mdai na anase vitu vyote alivyo navyo, Wageni na wateke mapato ya kazi yake.
12 Asiwe na mtu wa kumfanyia fadhili, Wala mtu wa kuwahurumia yatima wake.
13 Wazao wake waangamizwe, Jina lao likafutwe katika kizazi cha pili.
14 Uovu wa baba zake ukumbukwe mbele za Bwana, Na dhambi ya mamaye isifutwe.
15 Ziwe mbele za Bwana daima, Aliondoe kumbukumbu lao duniani.
16 Kwa kuwa hakukumbuka kutenda fadhili, Bali alimfukuza mnyonge na mhitaji, Hata akamfisha mtu aliyevunjika moyo,
17 Naye alipenda kulaani, nako kukampata. Hakupendezwa na kubariki, kukawa mbali naye,
18 Alijivika laana kana kwamba ni vazi lake. Ikamwingilia moyoni kama maji, Na kama mafuta mifupani mwake.
19 Na iwe kwake kama vazi ajivikalo, Na kama mshipi ajifungao daima.
20 Ndiyo malipo ya washitaki wangu toka kwa Bwana, Na ya hao wanaoisingizia nafsi yangu mabaya.
21 Na Wewe, MUNGU, Bwana, unitendee kwa ajili ya jina lako, Kwa kuwa fadhili zako ni njema uniokoe.
22 Kwa maana mimi ni mnyonge na mhitaji, Na moyo wangu umejeruhi ndani yangu.
23 Ninapita kama kivuli kianzacho kutoweka, Ninapeperushwa kama nzige.
24 Magoti yangu yamedhoofu kwa kufunga, Na mwili wangu umekonda kwa kukosa mafuta.
25 Nami nalikuwa laumu kwao, Wanionapo hutikisa vichwa vyao.
26 Ee Bwana, Mungu wangu, unisaidie, Uniokoe sawasawa na fadhili zako.
27 Nao wakajue ya kuwa ndio mkono wako; Wewe, Bwana, umeyafanya hayo.
28 Wao walaani, bali Wewe utabariki, Wameondoka wao wakaaibishwa, Bali mtumishi wako atafurahi.
29 Washitaki wangu watavikwa fedheha, Watajivika aibu yao kama joho.
30 Nitamshukuru Bwana kwa kinywa changu, Naam, nitamsifu katikati ya mkutano.
31 Maana atasimama mkono wa kuume wa mhitaji Amwokoe na wanaoihukumu nafsi yake.