Mithali 29
1 Aonywaye mara nyingi akishupaza shingo, Atavunjika ghafula, wala hapati dawa.
2 Wenye haki wakiwa na amri, watu hufurahi; Bali mwovu atawalapo, watu huugua.
3 Apendaye hekima humfurahisha babaye; Bali ashikamanaye na makahaba hutapanya mali.
4 Mfalme huithibitisha nchi kwa hukumu; Bali yeye apokeaye rushwa huipindua.
5 Mwenye kujipendekeza kwa jirani yake, Hutandika wavu ili kuitega miguu yake.
6 Kuna mtego katika kosa la mtu mbaya; Bali mwenye haki huimba na kufurahi.
7 Mwenye haki huyaangalia madai ya maskini; Bali mtu mbaya hana ufahamu hata ayajue.
8 Watu wenye dharau huwasha mji moto; Bali wenye hekima hugeuzia mbali ghadhabu.
9 Mwenye hekima akijadiliana na mpumbavu; Akikasirika au akicheka, pia hapana raha.
10 Wamwagao damu humchukia mtu mkamilifu; Bali wenye haki humtunza nafsi yake.
11 Mpumbavu hudhihirisha hasira yake yote; Bali mwenye hekima huizuia na kuituliza.
12 Mwenye kutawala akisikiliza uongo; Basi watumishi wake wote watakuwa waovu.
13 Maskini na mdhalimu hukutana pamoja; Bwana huwatia nuru macho yao wote wawili.
14 Mfalme awahukumuye maskini kwa uaminifu; Kiti chake cha enzi kitathibitika milele.
15 Fimbo na maonyo hutia hekima; Bali mwana aliyeachiliwa humwaibisha mamaye.
16 Waovu wakiongezeka, maasi huongezeka; Bali wenye haki watayatazama maanguko yao.
17 Mrudi mwanao naye atakustarehesha; Naam, atakufurahisha nafsi yako.
18 Pasipo maono, watu huacha kujizuia; Bali ana heri mtu yule aishikaye sheria.
19 Haitoshi mtumwa kuonywa kwa maneno; Maana ajapoyafahamu hataitika.
20 Je! Umemwona mtu mwenye kuhamaki katika maneno? Afadhali kumtumaini mpumbavu kuliko yeye.
21 Amtunduiaye mtumwa wake tangu utoto, Mwisho wake atakuwa ni mwanawe.
22 Mtu wa hasira huchochea ugomvi; Na mtu mwenye ghadhabu huasi sana.
23 Kiburi cha mtu kitamshusha; Bali mwenye roho ya unyenyekevu ataheshimiwa.
24 Mshiriki wa mwivi huichukia nafsi yake mwenyewe; Asikia maapizo, wala hana neno.
25 Kuwaogopa wanadamu huleta mtego; Bali amtumainiye Bwana atakuwa salama.
26 Watu wengi hutafuta upendeleo wa mkuu; Bali hukumu ya kila mtu hutoka kwa Bwana
27 Mtu aliye dhalimu ni chukizo kwa wenye haki; Na mnyofu wa mwenendo ni chukizo kwa waovu.