«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »

Mithali 21

1  Moyo wa mfalme huwa katika mkono wa Bwana; Kama mifereji ya maji huugeuza po pote apendapo.

2  Kila njia ya mtu ni sawa machoni pake mwenyewe; Bali Bwana huipima mioyo.

3  Kutenda haki na hukumu Humpendeza Bwana kuliko kutoa sadaka.

4  Macho yenye kiburi, na moyo wa kutakabari, Hata ukulima wa waovu, ni dhambi.

5  Mawazo ya wenye bidii huuelekea utajiri tu; Bali kila mwenye pupa huuelekea uhitaji.

6  Kupata akiba ya mali kwa ulimi wa uongo Ni moshi upeperushwao; ni kutafuta mauti.

7  Jeuri ya wabaya itawaondolea mbali; Kwa sababu wamekataa kutenda hukumu.

8  Njia yake aliyelemewa na dhambi imepotoka sana; Bali mtu aliye safi, kazi yake ni sawasawa.

9  Ni afadhali kukaa katika pembe ya darini, Kuliko katika nyumba pana pamoja na mwanamke mgomvi.

10  Nafsi ya mtu mbaya hutamani uovu; Jirani yake hapati fadhili machoni pake.

11  Mwenye mzaha aadhibiwapo, mjinga hupata hekima; Na mwenye hekima afundishwapo, hupokea maarifa.

12  Mwenye haki huitafakari nyumba ya mtu mbaya; Jinsi wabaya waangushwavyo wakaangamia.

13  Azibaye masikio yake asisikie kilio cha maskini, Yeye naye atalia, lakini hatasikiwa.

14  Kipawa cha siri hutuliza hasira; Na rushwa bindoni humliza ghadhabu kali.

15  Ni furaha yao wenye haki kutenda hukumu; Lakini ni uharibifu kwao watendao maovu.

16  Mtu aikosaye njia ya busara Atakaa katika mkutano wao waliokufa.

17  Mtu apendaye anasa atakuwa maskini; Apendaye mvinyo na mafuta hatakuwa tajiri.

18  Mtu asiye haki ni fidia ya wenye haki; Naye afanyaye hila ni badala ya watu wa adili.

19  Ni afadhali kukaa katika nchi ya nyika; Kuliko na mwanamke mgomvi, mchokozi.

20  Kuna hazina ya thamani na mafuta katika maskani ya mwenye hekima; Bali mwanadamu aliye mpumbavu huyameza.

21  Aandamaye haki na fadhili, Ataona uhai na haki na heshima.

22  Mwenye hekima huupandia mji wao wenye nguvu; Na kuziangusha nguvu za tumaini lao.

23  Mtu azuiaye kinywa chake na ulimi wake, Atajilinda nafsi yake na taabu.

24  Mwenye kiburi na kutakabari, jina lake ni mbishi; Hutenda mambo katika majivuno ya kiburi chake.

25  Matakwa yake mtu mvivu humfisha, Kwa maana mikono yake hukataa kufanya kazi.

26  Kuna atamaniye kwa choyo mchana kutwa; Bali mwenye haki hutoa wala hanyimi.

27  Sadaka ya wasio haki ni chukizo; Si zaidi sana ailetapo mwenye nia mbaya!

28  Shahidi wa uongo atapotea; Bali mtu asikiaye atasema maneno yadumuyo.

29  Asiye haki huufanya uso wake kuwa mgumu; Bali mtu mnyofu huzifikiri njia zake.

30  Hapana hekima, wala ufahamu, Wala shauri, juu ya Bwana.

31  Farasi huwekwa tayari kwa siku ya vita; Lakini Bwana ndiye aletaye wokovu.

«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »
“Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi.” — 1 Wakorintho 16:23