«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »

Mithali 20

1  Mvinyo hudhihaki, kileo huleta ugomvi; Na akosaye kwa vitu hivyo hana hekima.

2  Utisho wa mfalme ni kama ngurumo ya simba; Amkasirishaye huitendea dhambi nafsi yake.

3  Mtu kujitenga na ugomvi ni heshima kwake; Bali kila mpumbavu ataka kugombana.

4  Mtu mvivu hataki kulima wakati wa baridi; Hivyo wakati wa mavuno ataomba, hana kitu.

5  Mashauri ya moyoni ni kama kilindi; Lakini mtu mwenye ufahamu atayateka.

6  Wanadamu hutangaza kila mtu hisani yake mwenyewe; Bali mtu aliye mwaminifu, ni nani awezaye kumpata?

7  Mwenye haki aendaye katika unyofu wake, Watoto wake wabarikiwa baada yake.

8  Mfalme aketiye katika kiti cha hukumu, Huyapepeta mabaya yote kwa macho yake.

9  Nani awezaye kusema, Nimesafisha moyo wangu; Nimetakasika dhambi yangu?

10  Vipimo mbalimbali, na pishi mbalimbali, Vyote viwili ni chukizo kwa Bwana.

11  Hata mtoto hujijulisha kwa matendo yake; Kwamba kazi yake ni safi, kwamba ni adili.

12  Sikio lisikialo, na jicho lionalo, Bwana ndiye aliyeyafanya yote mawili.

13  Usipende usingizi usije ukawa maskini; Fumbua macho yako nawe utashiba chakula.

14  Haifai kitu, haifai kitu, asema mnunuzi; Lakini akiisha kwenda zake hujisifu.

15  Dhahabu iko, na marijani tele; Lakini midomo ya maarifa ni kito cha thamani.

16  Twaa nguo yake amdhaminiye mgeni; Mtoze rehani aliye mdhamini wa wageni.

17  Chakula cha uongo ni kitamu kwa mtu; Lakini halafu kinywa chake kitajaa changarawe.

18  Kila kusudi huthibitika kwa kushauriana; Na kwa shauri la akili fanya vita.

19  Mwenye kitango akisingizia hufunua siri; Basi, usishirikiane naye afunuaye midomo yake sana.

20  Amlaaniye babaye au mamaye, Taa yake itazimika katika giza kuu.

21  Urithi uliopatikana mwanzo kwa haraka, Mwisho wake, lakini, hautabarikiwa.

22  Usiseme, Mimi nitalipa mabaya; Mngojee Bwana, naye atakuokoa.

23  Vipimo mbalimbali ni chukizo kwa Bwana; Tena mizani ya hila si njema.

24  Mwenendo wa mtu watoka kwa Bwana; Basi, awezaje mtu kuelewa na njia yake?

25  Ni mtego, mtu aseme kwa haraka, Kitu hiki ni wakfu; Na baada ya kuweka nadhiri kuuliza-uliza habari.

26  Mfalme mwenye hekima huwapepeta wasio haki; Naye hulipitisha gurudumo la kupuria juu yao.

27  Pumzi ya mwanadamu ni taa ya Bwana; Hupeleleza yote yaliyomo ndani yake.

28  Fadhili na uaminifu humhifadhi mfalme, Na kiti chake cha enzi huthibitishwa kwa fadhili.

29  Fahari ya vijana ni nguvu zao, Na uzuri wa wazee ni kichwa chenye mvi.

30  Machubuko ya fimbo husafisha uovu, Na mapigo hufikilia ndani ya mtima.

«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »
“Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi.” — 1 Wakorintho 16:23