Mithali 18
1 Ajitengaye na wenzake hutafuta matakwa yake mwenyewe; Hushindana na kila shauri jema.
2 Mpumbavu hapendezwi na ufahamu; Ila moyo wake udhihirike tu.
3 Ajapo asiye haki, huja dharau pia; Na pamoja na aibu huja lawama.
4 Maneno ya kinywa cha mtu ni kama maji ya vilindi; Kijito kibubujikacho; chemchemi ya hekima.
5 Kukubali uso wake asiye haki si vizuri; Wala kumpotosha mwenye haki hukumuni.
6 Midomo ya mpumbavu huingia katika fitina, Na kinywa chake huita mapigo.
7 Kinywa cha mpumbavu ni uharibifu wake, Na midomo yake ni mtego wa nafsi yake.
8 Maneno ya mchongezi ni kama vitoweo; Nayo hushukia pande za ndani za tumbo.
9 Yeye naye aliye mvivu katika kazi yake, Ni ndugu yake aliye mharabu.
10 Jina la Bwana ni ngome imara; Mwenye haki huikimbilia, akawa salama.
11 Mali ya mtu tajiri ni mji wake wa nguvu; Ni kama ukuta mrefu katika mawazo yake.
12 Kabla ya uharibifu moyo wa mwanadamu hujivuna; Na kabla ya heshima hutangulia unyenyekevu.
13 Yeye ajibuye kabla hajasikia, Ni upumbavu na aibu kwake.
14 Roho ya mtu itastahimili udhaifu wake; Bali roho iliyovunjika nani awezaye kuistahimili?
15 Moyo wa mwenye busara hupata maarifa; Na sikio la mwenye hekima hutafuta maarifa.
16 Zawadi ya mtu humpatia nafasi; Humleta mbele ya watu wakuu.
17 Ajiteteaye kwanza huonekana kuwa ana haki; Lakini jirani yake huja na kumchunguza.
18 Kura hukomesha mashindano; Hukata maneno ya wakuu.
19 Ndugu aliyechukizwa ni mgumu kuliko mji wa nguvu; Na mashindano ni kama mapingo ya ngome.
20 Tumbo la mtu litajazwa matunda ya kinywa chake; Atashiba mazao ya midomo yake.
21 Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; Na wao waupendao watakula matunda yake.
22 Apataye mke apata kitu chema; Naye ajipatia kibali kwa Bwana.
23 Maskini hutumia maombi; Bali tajiri hujibu kwa ukali.
24 Ajifanyiaye rafiki wengi ni kwa uangamivu wake mwenyewe; Lakini yuko rafiki aambatanaye na mtu kuliko ndugu.