«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »

Mithali 15

1  Jawabu la upole hugeuza hasira; Bali neno liumizalo huchochea ghadhabu.

2  Ulimi wa mwenye hekima hutamka maarifa vizuri; Bali vinywa vya wapumbavu humwaga upumbavu.

3  Macho ya Bwana yako kila mahali; Yakimchunguza mbaya na mwema.

4  Ulimi safi ni mti wa uzima; Bali ukorofi wa ulimi huvunja moyo.

5  Mpumbavu hudharau kurudiwa na babaye; Bali yeye aangaliaye maonyo hupata busara.

6  Katika nyumba ya mwenye haki mna akiba nyingi; Bali mapato ya mtu mbaya huwa taabu tu.

7  Midomo ya mwenye haki hueneza maarifa; Bali moyo wa mpumbavu haufanyi hivyo.

8  Sadaka ya mtu mbaya ni chukizo kwa Bwana; Bali maombi ya mtu mnyofu ni furaha yake.

9  Njia ya mtu mbaya ni chukizo kwa Bwana; Bali humpenda mtu afuatiaye wema.

10  Adhabu kali ina yeye aiachaye njia; Naye achukiaye kukemewa atakufa.

11  Kuzimu na Uharibifu vi wazi mbele za Bwana; Si zaidi basi, mioyo ya wanadamu?

12  Mwenye mzaha hapendi kukaripiwa; Wala yeye hawaendei wenye hekima.

13  Moyo wa furaha huchangamsha uso; Bali kwa huzuni ya moyo roho hupondeka.

14  Moyo wa mwenye ufahamu hutafuta maarifa; Bali kinywa cha wapumbavu hula upumbavu.

15  Siku zote za mtu ateswaye ni mbaya; Bali ukunjufu wa moyo ni karamu ya daima.

16  Kuwa na mali chache pamoja na kumcha Bwana; Ni bora kuliko mali nyingi pamoja na taabu.

17  Chakula cha mboga penye mapendano; Ni bora kuliko ng'ombe aliyenona pamoja na kuchukiana.

18  Mtu wa hasira huchochea ugomvi; Bali asiye mwepesi wa hasira hutuliza mashindano.

19  Njia ya mtu mvivu ni kama boma la miiba; Bali mapito yao wenye unyofu hufanyika njia kuu.

20  Mwana mwenye hekima humfurahisha babaye; Bali mpumbavu humdharau mamaye.

21  Upumbavu ni furaha kwake aliyepungukiwa na akili; Bali mwenye ufahamu huunyosha mwenendo wake.

22  Pasipo mashauri makusudi hubatilika; Bali kwa wingi wa washauri huthibithika.

23  Mtu hulifurahia jibu la kinywa chake; Na neno linenwalo wakati wa kufaa ni jema kama nini!

24  Kwa mtu mwenye akili njia ya uhai huenda juu; Ili atoke katika kuzimu chini.

25  Bwana ataing'oa nyumba ya mwenye kiburi; Bali atauthibitisha mpaka wa mjane.

26  Mashauri mabaya ni chukizo kwa Bwana; Bali maneno yapendezayo ni safi.

27  Atamaniye faida huifadhaisha nyumba yake mwenyewe; Bali achukiaye zawadi ataishi.

28  Moyo wa mwenye haki hufikiri jinsi atakavyojibu; Bali kinywa cha wasio haki humwaga mabaya.

29  Bwana yu mbali na wasio haki; Bali huisikia sala ya mwenye haki.

30  Mng'ao wa macho huufurahisha moyo; Habari njema huinenepesha mifupa.

31  Sikio lisikilizalo lawama yenye uhai Litakaa kati yao wenye hekima.

32  Akataaye maonyo huidharau nafsi yake mwenyewe; Bali yeye asikilizaye lawama hujipatia ufahamu.

33  Kumcha Bwana ni maonyo ya hekima; Na kabla ya heshima hutangulia unyenyekevu.

«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »
“Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi.” — 1 Wakorintho 16:23