Mithali 14
1 Kila mwanamke aliye na hekima hujenga nyumba yake; Bali aliye mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe.
2 Yeye aendaye kwa unyofu wake humcha Bwana; Bali aliye mkaidi katika njia zake humdharau.
3 Katika kinywa cha mpumbavu mna fimbo ya kiburi, Bali midomo ya wenye hekima huwahifadhi.
4 Zizi ni safi ambapo hapana ng'ombe; Bali nguvu za ng'ombe zaleta faida nyingi.
5 Shahidi mwaminifu hatasema uongo; Bali shahidi wa uongo, pumzi zake ni uongo.
6 Mwenye dharau hutafuta hekima, asiipate; Bali maarifa huwa mepesi kwa mwenye ufahamu.
7 Toka mbele ya uso wa mpumbavu, Maana hutaona kwake midomo ya maarifa.
8 Akili za mwenye busara ni kujua njia yake; Lakini upumbavu wa wapumbavu ni udanganyifu.
9 Wapumbavu huidharau hatia; Bali upo upendeleo kwa wenye haki.
10 Moyo huujua uchungu wa nafsi yake, Wala mgeni haishiriki furaha yake.
11 Nyumba ya mtu mbaya itabomolewa; Bali hema ya mwenye haki itafanikiwa.
12 Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu, Lakini mwisho wake ni njia za mauti.
13 Hata wakati wa kucheka moyo huwa na huzuni; Na mwisho wa furaha ni uzito wa moyo.
14 Ageukaye moyoni hushiba njia zake mwenyewe; Na mtu mwema ataridhika nafsini mwake.
15 Mjinga huamini kila neno; Bali mwenye busara huangalia sana aendavyo.
16 Mwenye hekima huogopa, akajitenga na uovu; Bali mpumbavu ana ufidhuli, na kujitumai.
17 Yeye aonaye hasira upesi atatenda kwa ujinga; Na mtu mwenye hila mbaya huzirwa.
18 Wajinga hurithi upumbavu; Bali wenye busara huvikwa taji ya maarifa.
19 Wabaya huinama mbele ya wema, Na wasio haki malangoni mwao wenye haki.
20 Maskini huchukiwa hata na jirani yake; Bali tajiri ana rafiki wengi.
21 Amdharauye mwenzake afanya dhambi; Bali amhurumiaye maskini ana heri.
22 Je! Hawakosi wawazao mabaya? Bali fadhili na kweli zina wao wawazao mema.
23 Katika kila kazi mna faida; Bali maneno ya midomo huleta hasara tu.
24 Taji ya wenye hekima ni mali zao; Bali upumbavu wa wajinga ni upumbavu tu.
25 Shahidi wa kweli huponya nafsi za watu; Bali atoaye uongo hudanganya.
26 Kumcha Bwana ni tumaini imara; Watoto wake watakuwa na kimbilio.
27 Kumcha Bwana ni chemchemi ya uzima, Ili kuepukana na tanzi za mauti.
28 Utukufu wa mfalme ni wingi wa watu wake; Bali uchache wa watu ni uharibifu wa mkuu wao.
29 Asiye mwepesi wa hasira ana fahamu nyingi; Bali mwenye roho ya hamaki hutukuza upumbavu.
30 Moyo ulio mzima ni uhai wa mwili; Bali husuda ni ubovu wa mifupa.
31 Amwoneaye maskini humsuta Muumba wake; Bali yeye awahurumiaye wahitaji humheshimu.
32 Mtu mbaya husukumwa chini katika kutenda mabaya kwake; Bali mwenye haki ana matumaini katika kufa kwake.
33 Hekima hukaa katika moyo wake mwenye ufahamu; Bali yaliyo ndani ya wapumbavu hudhihirika.
34 Haki huinua taifa; Bali dhambi ni aibu ya watu wo wote.
35 Upendeleo wa mfalme humwelekea mtumwa atendaye kwa busara; Bali ghadhabu yake itakuwa juu yake aletaye aibu.