Mithali 13
1 Mwana mwenye hekima husikiliza mausia ya babaye; Bali mwenye dharau hasikilizi maonyo.
2 Mtu atakula mema kwa matunda ya kinywa chake; Bali nafsi ya mtu haini itakula jeuri.
3 Yeye alindaye kinywa chake huilinda nafsi yake; Bali afunuaye midomo yake atapata uharibifu.
4 Nafsi ya mtu mvivu hutamani asipate kitu; Bali nafsi ya mwenye bidii itanenepeshwa.
5 Mwenye haki huchukia kusema uongo; Bali mtu mbaya huwa karaha, hupatwa na aibu.
6 Haki humlinda yeye aliye mnyofu katika njia yake; Bali ubaya humwangusha mwenye dhambi.
7 Kuna mtu mwenye kujitajirisha, lakini hana kitu; Kuna ajifanyaye kuwa maskini, lakini ana mali nyingi.
8 Dia ya nafsi ya mtu ni utajiri wake; Bali mtu maskini hasikii ogofyo lo lote.
9 Nuru ya mwenye haki yang'aa sana; Bali taa ya mtu mbaya itazimika.
10 Kiburi huleta mashindano tu; Bali hekima hukaa nao wanaoshauriana.
11 Mali iliyopatikana kwa haraka itapunguka; Bali yeye achumaye kidogo kidogo atazidishiwa.
12 Kilichotarajiwa kikikawia kuja, moyo huugua. Bali haja ya mtu ikipatikana, ni mti wa uzima.
13 Kila alidharauye neno hujiletea uharibifu; Bali yeye aiogopaye amri atapewa thawabu.
14 Sheria ya mwenye akili ni chemchemi ya uzima, Ili kuepukana na tanzi za mauti.
15 Ufahamu mwema huleta upendeleo; Bali njia ya haini huparuza.
16 Kila aliye na busara hutenda kazi kwa maarifa; Bali mpumbavu hueneza upumbavu.
17 Mjumbe mbaya huanguka maovuni; Bali mjumbe mwaminifu ni afya.
18 Umaskini na fedheha zitampata yeye akataaye kurudiwa; Bali yeye aangaliaye maonyo ataheshimiwa.
19 Haja iliyopatikana ni tamu nafsini mwa mtu; Bali kujitenga na maovu ni chukizo kwa wapumbavu.
20 Enenda pamoja na wenye hekima, nawe utakuwa na hekima; Bali rafiki wa wapumbavu ataumia.
21 Uovu huwaandamia wenye dhambi; Bali mwenye haki atalipwa mema.
22 Mtu mwema huwaachia wana wa wanawe urithi; Na mali ya mkosaji huwa akiba kwa mwenye haki.
23 Chakula kingi chapatikana kwa ukulima wa maskini; Bali viko viharibiwavyo kwa sababu ya dhuluma.
24 Yeye asiyetumia fimbo yake humchukia mwanawe; Bali yeye ampendaye humrudi mapema.
25 Mwenye haki hula akaishibisha nafsi yake; Bali tumbo la mtu mbaya litaona njaa.