«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »

Mithali 12

1  Kila apendaye mafundisho hupenda maarifa; Bali yeye achukiaye kulaumiwa ni kama mnyama.

2  Mtu mwema atapata upendeleo kwa Bwana; Bali mtu wa hila atahukumiwa naye.

3  Mtu hatathibitika kwa njia ya uovu; Shina la mwenye haki halitaondolewa kamwe.

4  Mwanamke mwema ni taji ya mumewe; Bali aaibishaye ni kama kuoza mifupani mwake.

5  Mawazo ya mwenye haki ni adili; Bali mashauri ya mtu mwovu ni hadaa.

6  Maneno ya waovu huotea damu; Bali kinywa cha wanyofu kitawaokoa.

7  Waovu huangamia, hata hawako tena; Bali nyumba ya mwenye haki itasimama.

8  Mtu atasifiwa kwa kadiri ya akili zake; Bali mwenye moyo wa ukaidi atadharauliwa.

9  Afadhali mtu anayedharauliwa, ikiwa ana mtumwa, Kuliko ajisifuye, ikiwa anahitaji chakula.

10  Mwenye haki huufikiri uhai wa mnyama wake; Bali huruma za mtu mwovu ni ukatili.

11  Alimaye shamba lake atakuwa na chakula tele; Bali afuataye mambo ya upuzi hana ufahamu.

12  Asiye haki hutamani nyavu za wabaya; Bali shina lao wenye haki huleta matunda.

13  Katika kosa la midomo kuna mtego kwa mbaya; Bali mwenye haki atatoka katika taabu.

14  Mtu atashiba mema kwa matunda ya kinywa chake; Na atarudishiwa matendo ya mikono yake.

15  Njia ya mpumbavu imenyoka machoni pake mwenyewe; Bali yeye aliye na hekima husikiliza shauri.

16  Ghadhabu ya mpumbavu hujulika mara; Bali mtu mwerevu husitiri aibu.

17  Atamkaye maneno ya kweli hufunua haki; Bali shahidi wa uongo hutamka hila.

18  Kuna anenaye bila kufikiri, kama kuchoma kwa upanga; Bali ulimi wa mwenye haki ni afya.

19  Mdomo wa kweli utathibitishwa milele; Bali ulimi wa uongo ni wa kitambo tu.

20  Hila imo mioyoni mwao wafikirio uovu; Bali wafanyao mashauri ya amani, kwao kuna furaha.

21  Mwenye haki hatapatikana na msiba wo wote; Bali wasio haki watajazwa mabaya.

22  Midomo ya uongo ni chukizo kwa Bwana; Bali watendao uaminifu ndio furaha yake.

23  Mwanadamu mwenye busara husitiri maarifa; Bali moyo wa wapumbavu hutangaza upumbavu.

24  Mkono wa mwenye bidii utatawala; Bali mvivu atalipishwa kodi.

25  Uzito katika moyo wa mtu huuinamisha; Bali neno jema huufurahisha.

26  Mwenye haki ni kiongozi cha mwenzake; Bali njia ya wasio haki huwakosesha.

27  Mtu mvivu hapiki mawindo yake; Bali mwenye bidii anazo mali za thamani.

28  Katika njia ya haki kuna uhai; Wala hakuna mauti katika mapito yake.

«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »
“Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi.” — 1 Wakorintho 16:23