«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »

Mithali 10

1  Mwana mwenye hekima humfurahisha babaye; Bali mwana mpumbavu ni mzigo wa mamaye.

2  Hazina za uovu hazifaidii kitu; Bali haki huokoa na mauti.

3  Bwana hataiacha nafsi ya mwenye haki ife na njaa; Bali tamaa ya mtu mwovu huisukumia mbali.

4  Atendaye mambo kwa mkono mlegevu huwa maskini; Bali mkono wake aliye na bidii hutajirisha.

5  Akusanyaye wakati wa hari ni mwana mwenye hekima; Bali asinziaye wakati wa mavuno ni mwana mwenye kuaibisha.

6  Baraka humkalia mwenye haki kichwani; Bali jeuri hufunika kinywa chake mtu mwovu.

7  Kuwakumbuka wenye haki huwa na baraka; Bali jina la mtu mwovu litaoza.

8  Aliye na akili moyoni mwake atapokea agizo; Bali mpumbavu mwenye maneno mengi ataanguka.

9  Aendaye kwa unyofu huenda salama; Bali apotoshaye njia zake atajulikana.

10  Akonyezaye kwa jicho huleta masikitiko; Bali mpumbavu mwenye maneno mengi ataanguka.

11  Kinywa chake mwenye haki ni chemchemi ya uzima; Bali jeuri hufunika kinywa chake mtu mwovu,

12  Kuchukiana huondokesha fitina; Bali kupendana husitiri makosa yote.

13  Hekima hupatikana midomoni mwa mwenye ufahamu; Bali fimbo hufaa kwa mgongo wake asiye na ufahamu.

14  Watu wenye akili huweka akiba ya maarifa; Bali kinywa cha mpumbavu ni uangamivu ulio karibu.

15  Mali ya mtu tajiri ni mji wake wa nguvu; Uangamivu wa maskini ni umaskini wao.

16  Kazi yake mwenye haki huuelekea uzima; Mazao ya wabaya huuelekea dhambi.

17  Akubaliye kurudiwa huwa katika njia ya uzima; Bali yeye aachaye maonyo hukosa.

18  Yeye afichaye chuki ana midomo ya uongo, Na yeye asingiziaye ni mpumbavu.

19  Katika wingi wa maneno hapakosi kuwa na maovu; Bali yeye azuiaye midomo yake hufanya akili.

20  Ulimi wa mwenye haki ni kama fedha teule; Moyo wa mtu mbaya haufai kitu.

21  Midomo ya mwenye haki hulisha watu wengi; Bali wapumbavu hufa kwa kuwa hawana ufahamu.

22  Baraka ya Bwana hutajirisha, Wala hachanganyi huzuni nayo.

23  Kwa mpumbavu kutenda maovu ni kama mchezo; Bali mtu mwenye ufahamu ana hekima.

24  Aogopacho mtu asiye haki ndicho kitakachomjilia; Na wenye haki watapewa matakwa yao.

25  Kisulisuli kikiisha pita asiye haki hayuko tena; Bali mwenye haki ni msingi wa milele.

26  Kama siki menoni, na kama moshi machoni, Ndivyo alivyo mtu mvivu kwao wamtumao.

27  Kumcha Bwana kwaongeza siku za mtu; Bali miaka yao wasio haki itapunguzwa.

28  Matumaini yao wenye haki yatakuwa furaha; Bali kutaraji kwao wasio haki kutapotea.

29  Njia ya Bwana ni kimbilio lake mtu mkamilifu; Bali ni uharibifu kwao watendao maovu.

30  Mwenye haki hataondolewa milele; Bali wasio haki hawatakaa katika nchi.

31  Kinywa cha mwenye haki hutoa hekima; Bali ulimi wa ukaidi utakatiliwa mbali.

32  Midomo ya mwenye haki huyajua yatakayokubaliwa; Bali kinywa chao wasio haki hunena ukaidi.

«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »
“Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi.” — 1 Wakorintho 16:23