«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »

Mithali 1

1  Mithali za Sulemani, mwana wa Daudi, mfalme wa Israeli.

2  Kujua hekima na adabu; kutambua maneno ya ufahamu;

3  kufundishwa matendo ya busara, katika haki na hukumu na adili.

4  Kuwapa wajinga werevu, na kijana maarifa na hadhari;

5  mwenye hekima asikie na kuongezewa elimu, na mwenye ufahamu ayafikie mashauri yenye njia.

6  Kufahamu mithali na kitendawili, na maneno ya wenye hekima na mafumbo yao.

7  Kumcha Bwana ni chanzo cha maarifa, Bali wapumbavu hudharau hekima na adabu.

8  Mwanangu, yasikilize mafundisho ya baba yako, Wala usiiache sheria ya mama yako,

9  Kwa maana hayo yatakuwa kilemba cha neema kichwani pako, Na mikufu shingoni mwako.

10  Mwanangu, wenye dhambi wakikushawishi, Wewe usikubali.

11  Wakisema, Haya! Njoo pamoja nasi, Na tuvizie ili kumwaga damu; Tumwotee asiye na hatia, bila sababu;

12  Tuwameze hai kama kuzimu, Na wazima, kama wao washukao shimoni.

13  Tutapata mali yote ya thamani, Tutazijaza nyumba zetu mateka.

14  Wewe utashirikiana nasi; Tutakuwa na vitu vyote shirika.

15  Mwanangu, usiende njiani pamoja nao; Uzuie mguu wako usiende katika mapito yao.

16  Maana miguu yao huenda mbio maovuni, Nao hufanya haraka ili kumwaga damu.

17  Kwa kuwa mtego hutegwa bure, Mbele ya macho ya ndege ye yote.

18  Na hao hujiotea damu yao wenyewe, Hujinyemelea nafsi zao wenyewe.

19  Ndivyo zilivyo njia za kila mwenye tamaa ya mali; Huuondoa uhai wao walio nayo.

20  Hekima hupaza sauti yake katika njia kuu, Hutoa sauti yake katika viwanja;

21  Hulia penye mikutano mikubwa ya watu, Mahali pa kuyaingilia malango, Ndani ya mji hutamka maneno yake.

22  Enyi wajinga, hata lini mtapenda ujinga? Na wenye dharau kupenda dharau yao, Na wapumbavu kuchukia maarifa?

23  Geukeni kwa ajili ya maonyo yangu; Tazama, nitawamwagia roho yangu, Na kuwajulisheni maneno yangu.

24  Kwa kuwa nimeita, nanyi mkakataa; Nimeunyosha mkono wangu, asiangalie mtu;

25  Bali mmebatilisha shauri langu, Wala hamkutaka maonyo yangu;

26  Mimi nami nitacheka siku ya msiba wenu, Nitadhihaki hofu yenu ifikapo;

27  Hofu yenu ifikapo kama tufani, Na msiba wenu ufikapo kama kisulisuli, Dhiki na taabu zitakapowafikia.

28  Ndipo watakaponiita, lakini sitaitika; Watanitafuta kwa bidii, wasinione.

29  Kwa kuwa walichukia maarifa, Wala hawakuchagua kumcha Bwana.

30  Hawakukubali mashauri yangu, Wakayadharau maonyo yangu yote.

31  Kwa hiyo watakula matunda ya njia yao, Watashiba mashauri yao wenyewe.

32  Maana kurudi nyuma kwao wajinga kutawaua, Na kufanikiwa kwao wapumbavu kutawaangamiza.

33  Bali kila anisikilizaye atakaa salama, Naye atatulia bila kuogopa mabaya.

«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »
“Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi.” — 1 Wakorintho 16:23