«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »

Wafilipi 3

1  Hatimaye, ndugu zangu, furahini katika Bwana. Kuwaandikieni mambo yale yale hakuniudhi mimi, bali kutawafaa ninyi.

2  Jihadharini na mbwa, jihadharini na watendao mabaya, jihadharini na wajikatao.

3  Maana sisi tu tohara, tumwabuduo Mungu kwa Roho, na kuona fahari juu ya Kristo Yesu, wala hatuutumainii mwili.

4  Walakini mimi ningeweza kuutumainia mwili. Mtu ye yote akijiona kuwa anayo sababu ya kuutumainia mwili, mimi zaidi.

5  Nalitahiriwa siku ya nane, ni mtu wa taifa la Israeli, wa kabila ya Benyamini, Mwebrania wa Waebrania, kwa habari ya kuishika torati, ni Farisayo,

6  kwa habari ya juhudi, mwenye kuliudhi Kanisa, kwa habari ya haki ipatikanayo kwa sheria sikuwa na hatia.

7  Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, naliyahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo.

8  Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate Kristo;

9  tena nionekane katika yeye, nisiwe na haki yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria, bali ile ipatikanayo kwa imani iliyo katika Kristo, haki ile itokayo kwa Mungu, kwa imani;

10  ili nimjue yeye, na uweza wa kufufuka kwake, na ushirika wa mateso yake, nikifananishwa na kufa kwake;

11  ili nipate kwa njia yo yote kuifikia kiyama ya wafu.

12  Si kwamba nimekwisha kufika, au nimekwisha kuwa mkamilifu; la! Bali nakaza mwendo ili nipate kulishika lile ambalo kwa ajili yake nimeshikwa na Kristo Yesu.

13  Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele;

14  nakaza mwendo, niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu.

15  Basi sisi tulio wakamilifu na tuwaze hayo; na hata mkiwaza mengine katika jambo lo lote, Mungu atawafunulia hilo nalo.

16  Lakini, hapo tulipofika na tuenende katika lilo hilo.

17  Ndugu zangu, mnifuate mimi, mkawatazame wao waendao kwa kuufuata mfano tuliowapa ninyi.

18  Maana wengi huenenda, ambao nimewaambieni mara nyingi habari zao, na sasa nawaambia hata kwa machozi, kuwa ni adui za msalaba wa Kristo;

19  mwisho wao ni uharibifu, mungu wao ni tumbo, utukufu wao u katika fedheha yao, waniao mambo ya duniani.

20  Kwa maana sisi, wenyeji wetu uko mbinguni; kutoka huko tena tunamtazamia Mwokozi, Bwana Yesu Kristo;

21  atakayeubadili mwili wetu wa unyonge, upate kufanana na mwili wake wa utukufu, kwa uweza ule ambao kwa huo aweza hata kuvitiisha vitu vyote viwe chini yake.

«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »
“Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi.” — 1 Wakorintho 16:23