Hesabu 32
1 Basi wana wa Reubeni, na hao wana wa Gadi, walikuwa na wanyama wa mifugo wengi sana; nao walipoona nchi ya Yazeri, na nchi ya Gileadi, ya kuwa mahali hapo palikuwa ni mahali pa kuwafaa wanyama;
2 hao wana wa Gadi, na wana wa Reubeni, wakamwendea Musa na Eleazari kuhani, na wakuu wa mkutano, wakanena nao, wakisema,
3 Atarothi, na Diboni, na Yazeri, na Nimra, na Heshboni, na Eleale, na Sebamu, na Nebo na Beoni,
4 nchi hiyo ambayo Bwana aliipiga mbele ya mkutano wa Israeli, ni nchi ifaayo kwa mfugo wa wanyama, nasi watumishi wako tuna wanyama.
5 Wakasema, Kama tumepata kibali mbele ya macho yako, sisi watumishi wako na tupewe nchi hii iwe milki yetu; usituvushe mto wa Yordani.
6 Musa akawaambia wana wa Gadi na wana wa Reubeni, Je! Ndugu zenu waende vitani nanyi mtaketi hapa?
7 Mbona mwawavunja mioyo yao wana wa Israeli, wasivuke na kuingia nchi hiyo ambayo Bwana amewapa?
8 Ndivyo walivyofanya baba zenu, hapo nilipowatuma kutoka Kadesh-barnea ili waende kuiangalia hiyo nchi.
9 Kwa kuwa walipokwea na kuingia bonde la Eshkoli, na kuiona nchi, wakawavunja mioyo wana wa Israeli, ili wasikwee kuingia nchi Bwana aliyowapa.
10 Na siku ile hasira za Bwana ziliwaka, naye akaapa, akisema,
11 Hakika yangu hapana mtu mmoja katika wale watu waliotoka Misri, tangu huyo aliyepata umri wa miaka ishirini, na zaidi, atakayeiona hiyo nchi niliyomwapia Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo; kwa sababu hawakuniandama kwa moyo wote;
12 ila Kalebu mwana wa Yefune, Mkenizi, na Yoshua mwana wa Nuni; kwa kuwa wao wamemwandama Bwana kwa moyo wote.
13 Na hasira za Bwana ziliwaka juu ya Israeli, naye akawatembeza huku na huku jangwani muda wa miaka arobaini, hata kizazi hicho kizima kilichokuwa kimefanya uovu machoni pa Bwana kikaisha angamia.
14 Na tazama, ninyi mmeinuka badala ya baba zenu, maongeo ya watu wenye dhambi, ili kuongeza tena hizo hasira kali za Bwana juu ya Israeli.
15 Kwa kuwa mkigeuka msimwandame, yeye atawaacha tena nyikani; nanyi mtawaangamiza watu hawa wote.
16 Basi wakamwendea karibu, na kusema, Sisi tutafanya mazizi hapa kwa ajili ya wanyama wetu wa mifugo, na kujenga miji kwa ajili ya watoto wetu;
17 lakini sisi wenyewe tutakuwa tayari na silaha zetu kutangulia mbele ya wana wa Israeli, hata tutakapowafikisha mahali pao; na watoto wetu watakaa katika hiyo miji yenye maboma, kwa sababu ya wenyeji wa nchi.
18 Sisi hatutarudia nyumba zetu, hata wana wa Israeli watakapokuwa wamekwisha kurithi kila mtu urithi wake.
19 Kwa kuwa sisi hatutarithi pamoja nao huko ng'ambo ya pili ya Yordani, huko mbele; kwa sababu urithi wetu umetuangukia upande huu wa Yordani kwa mashariki.
20 Basi Musa akawaambia, Kama mtafanya jambo hili; kama mtajivika silaha, ili kutangulia mbele ya Bwana mwende vitani,
21 tena kama kila mume wa kwenu mwenye kuchukua silaha atavuka Yordani mbele ya Bwana, hata atakapokuwa amekwisha watoa adui zake mbele yake,
22 na hiyo nchi kushindwa mbele za Bwana; ndipo baadaye mtarudi, nanyi mtakuwa hamna hatia mbele za Bwana, wala kwa Israeli; na nchi hii itakuwa milki yenu mbele za Bwana.
23 Lakini kama hamtaki kufanya neno hilo, ninyi mmefanya dhambi mbele za Bwana, nanyi jueni ya kwamba hiyo dhambi yenu itawapata hapana budi.
24 Basi, jengeni miji kwa ajili ya watoto wenu, na mazizi kwa ajili ya kondoo zenu; mkayafanye hayo mliotamka kwa vinywa vyenu.
25 Ndipo wana wa Gadi na wana wa Reubeni wakanena na Musa, na kumwambia, Sisi watumishi wako tutafanya kama wewe bwana wangu utuagizavyo.
26 Watoto wetu, na wake wetu, na kondoo zetu, na ng'ombe zetu wote, watakuwa hapo katika miji ya Gileadi;
27 lakini sisi watumishi wako tutavuka, kila mume aliyevaa silaha za vita, mbele za Bwana, tuende vitani, kama wewe bwana wangu usemavyo.
28 Basi Musa akamwagiza Eleazari kuhani, na Yoshua mwana wa Nuni, na wakuu wa nyumba za mababa za kabila za wana wa Israeli, katika habari za watu hao.
29 Musa akawaambia, Kwamba wana wa Gadi, na wana wa Reubeni, watavuka Yordani pamoja nanyi, kila mtu aliyevaa silaha kwa vita, mbele za Bwana, nayo nchi itashindwa mbele yenu; ndipo mtawapa nchi ya Gileadi kuwa milki yao;
30 lakini ikiwa hawataki kuvuka pamoja nanyi, hali wamevaa silaha zao, ndipo watakuwa na milki zao kati yenu katika nchi ya Kanaani.
31 Wana wa Gadi, na wana wa Reubeni, wakajibu na kusema, Kama Bwana alivyotuambia sisi watumishi wako, ndivyo tutakavyofanya.
32 Tutavuka, hali tumevaa silaha zetu, mbele za Bwana, kuingia nchi ya Kanaani, nayo milki ya urithi wetu itakuwa ng'ambo ya pili ya Yordani.
33 Basi Musa akawapa wao, maana, wana wa Gadi, na wana wa Reubeni, na hiyo nusu ya kabila ya Manase, mwana wa Yusufu, ufalme wa Sihoni mfalme wa Waamori, na ufalme wa Ogu mfalme wa Bashani, hiyo nchi, kama miji yao ilivyokuwa, pamoja na mipaka yake, maana, miji ya hiyo nchi iliyozunguka kotekote.
34 Kisha wana wa Gadi wakajenga Diboni, na Atarothi, na Aroeri;
35 na Atrothi-shofani, na Yazeri, na Yogbeha;
36 na, Beth-nimra, na Beth-harani; miji yenye maboma, na mazizi ya kondoo.
37 Na wana wa Reubeni wakajenga Heshboni, na Eleale, na Kiriathaimu;
38 na Nebo, na Baal-meoni, (majina yake yalikuwa yamegeuzwa) na Sibma; nao wakaiita miji waliyoijenga majina mengine.
39 Na wana wa Makiri mwana wa Manase wakaenda Gileadi, na kuitwaa, na kuwapokonya Waamori waliokuwamo humo.
40 Basi Musa akampa Makiri, mwana wa Manase, Gileadi, naye akakaa humo.
41 Kisha Yairi mwana wa Manase akaenda na kuvitwaa vijiji vya Gileadi. Akaviita jina lake Hawoth-yairi.
42 Kisha Noba akaenda na kutwaa Kenathi na vijiji vyake, na kuita jina lake Noba, kwa kuandama jina lake mwenyewe.